Serikali imesema Tanzania inakabiliwa na pengo la takribani dola bilioni 10 za Marekani katika fedha zinazohitajika kutekeleza mipango yake ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema hayo leo, Oktoba 5, 2026, wakati wa Mkutano wa Wadau wa Fedha za Tabianchi uliohusisha Serikali, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), wafadhili na washirika wa maendeleo.

Amesema Tanzania imeainisha mahitaji yake ya kifedha katika ahadi ilizojiwekea kimataifa, ambapo inahitaji takribani dola bilioni 19 kutekeleza hatua mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, amesema bado haijapata fedha za kutosha kutekeleza mipango hiyo, hali inayosababisha kuwepo kwa pengo la takribani dola bilioni 10.

“Tumishaanda commitment zetu kama taifa kwa ujumla kwa dunia ambapo tulibainisha kwamba tutahitaji angalau dola bilioni 19 kutekeleza hatua zote ambazo tulipanga kama taifa. Lakini ukiangalia ndani yake tukawa tuna gap, bado kuna fedha ambazo hazijapatikana kutekeleza,” amesema Balozi Omar.

Amesema Serikali imeendelea kuingiza masuala ya tabianchi katika mipango yake ya maendeleo, ikiwamo kuandaa Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (National Adaptation Plan), unaozingatia athari za tabianchi katika sekta mbalimbali.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mabadiliko ya tabianchi tayari yanaathiri miundombinu, kilimo na uzalishaji wa nishati, hivyo miradi ya maendeleo inapaswa kuzingatia changamoto hizo tangu hatua za awali za mipango.

Katika sekta ya nishati, amesema Tanzania imejiwekea lengo la kuhakikisha asilimia 75 ya nishati inatokana na vyanzo jadidifu, huku akieleza kuwa hadi sasa nchi imefikia asilimia 68.

Aidha, amesema Tanzania imeweka lengo la kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi kwa kati ya asilimia 30 na 35 ifikapo mwaka 2030, licha ya mchango wa nchi hiyo katika uzalishaji wa hewa chafuzi duniani kuwa takribani asilimia 0.31.

Balozi Omar amesema changamoto ya upatikanaji wa fedha za tabianchi si ya Tanzania pekee, bali ni suala linaloendelea kujadiliwa katika mikutano mbalimbali ya kimataifa.

Amesema mataifa yaliyoendelea yameahidi kuongeza fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutoka kiwango cha dola bilioni 300 kuelekea dola trilioni moja.

“Ni kitu kimoja kuwa na ahadi, lakini tunatarajia waweze kutimiza hizo ahadi,” amesema.

Amesema Tanzania itaendelea kuchukua hatua zake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, lakini inahitaji ushirikiano wa kimataifa ili mipango hiyo iweze kupata fedha na kutekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mazoezi wa Kanda wa Benki ya Dunia, Anna Wellenstein, amesema ajenda ya tabianchi nchini Tanzania ni sehemu ya ajenda ya maendeleo kutokana na athari zake ambazo tayari zinaonekana katika kilimo, maji, maeneo ya pwani, miundombinu, nishati na maisha ya wananchi.

Amesema ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha kuwa bila kuchukua hatua madhubuti, mabadiliko ya tabianchi yanaweza kupunguza ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa hadi asilimia nne ifikapo mwaka 2050.

“Tanzania ina msingi mzuri wa sera kupitia Dira ya Maendeleo na Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Tabianchi na mipango ya kisekta, lakini inahitaji kuweka vipaumbele, kuandaa miradi inayoweza kupata fedha na kutumia aina sahihi za fedha,” amesema Wellenstein.

Naye Mkurugenzi Msaidizi na Mkuu wa Ujumbe wa IMF, Nicolas Blancher, amesema Tanzania imeonyesha uongozi katika kuingiza masuala ya tabianchi katika ajenda yake ya maendeleo.

Amesema IMF imeisaidia Tanzania katika mageuzi yanayohusiana na kukabiliana na tabianchi, ikiwamo usimamizi wa majanga, uratibu wa taasisi na kuingiza masuala ya tabianchi katika mipango ya uwekezaji wa umma.

Blancher amesema mafanikio katika eneo hilo yanahitaji uongozi wa nchi, uratibu wa wadau, majukumu yaliyo wazi pamoja na mipango yenye muda maalumu wa utekelezaji.