Ndugu Wanachama, Viongozi, Wataalamu wa Tiba Asili, Wadau wa Afya na Mazingira, pamoja na Watanzania wote,
Kwa heshima na unyenyekevu, ninawasalimu na kuwapongeza wote wanaojitoa katika kuwahudumia wananchi na jamii kwa ujumla.
Tunapoadhimisha Wiki ya Huduma 2026, ninapenda kusisitiza kwamba huduma siyo kazi au wajibu wa mtu mmoja pekee; ni dhamana ya pamoja inayohitaji moyo wa kujitolea, upendo, uadilifu, weledi, huruma na uwajibikaji.
Kwa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania, Wiki ya Huduma ni fursa ya kutafakari namna tunavyoweza kuboresha huduma zetu, kuimarisha mshikamano wetu na kuongeza mchango wetu katika afya ya jamii na ulinzi wa mazingira.
TIBA ASILI NI HUDUMA YENYE DHAMANA
Ndugu Wanachama,
Kila mgonjwa anayemtafuta mtaalamu wa tiba asili huja akiwa na imani na matumaini. Imani hiyo ni dhamana kubwa inayopaswa kulindwa kwa uadilifu na uwajibikaji.
Kwa hiyo, ninawasihi wataalamu wa tiba asili nchini kutoa huduma kwa kuzingatia:
Usalama wa mgonjwa, usafi, ubora wa dawa, maadili, weledi, heshima na uwajibikaji.
Tuwe wataalamu wanaosikiliza wagonjwa, wanaojifunza, wanaofanya tafiti na wanaoshirikiana na wataalamu wengine wa afya pale inapohitajika.
Kwa pamoja, tukatae vitendo vinavyoweza kuhatarisha afya ya wananchi, ikiwemo ulaghai, ramli, ushirikina na ahadi zisizo na msingi wa kitaalamu.
AFYA YA BINADAMU NA AFYA YA MAZINGIRA
Kama Shirika linalounganisha dawa asilia na ulinzi wa mazingira, tunaamini kwamba afya ya binadamu haiwezi kutenganishwa na afya ya mazingira.
Maji safi, udongo salama, hewa safi, misitu, mimea tiba na bioanuwai ni sehemu ya msingi wa maisha na afya ya jamii.
Kwa hiyo, ninatoa wito kwa kila mtaalamu wa tiba asili kuwa mlezi wa mazingira, kutumia rasilimali za asili kwa uangalifu na kushiriki katika uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
TUWE SHIRIKA LA FARaja, UPENDO NA MSHIKAMANO
Huduma haipaswi kuishia katika kutoa tiba pekee.
Huduma ni pia kumfariji aliyefiwa, kumtia moyo mgonjwa, kumsaidia anayepitia changamoto na kusimama pamoja na mwenzetu wakati wa shida.
Ninawaomba wanachama wote tuendelee kujenga utamaduni wa kusaidiana na kuwa faraja kwa wengine.
Tukumbuke:
“Aheri kutoa kuliko kupokea.”
Mshikamano wetu katika nyakati ngumu ndiyo unaodhihirisha thamani ya uanachama wetu na upendo wetu kwa jamii.
WITO KWA VIONGOZI WA SHIRIKA
Kwa viongozi wenzangu katika ngazi zote, ninawasihi tuwe viongozi wa kutumikia, kusikiliza na kutatua changamoto za wanachama, badala ya kutafuta kutumikiwa.
Kila kiongozi awe mfano wa uadilifu, uwajibikaji, usawa na heshima.
Tujenge Shirika ambalo mwanachama anajivunia kuwa sehemu yake; Shirika linalosikiliza wataalamu wake; na Shirika linalotambulika kwa mchango wake katika afya, mazingira na maendeleo ya jamii.
WITO KWA WANACHAMA
Ndugu Wanachama,
Nguvu ya Shirika letu haitokani na jina lake pekee; nguvu yake inatokana na umoja, mshikamano, nidhamu na ushiriki wa kila mwanachama.
Ninawaomba tushirikiane, tuheshimiane, tutimize wajibu wetu na tushiriki kikamilifu katika shughuli za Shirika.
Tusijenge Shirika la viongozi pekee; tujenge Shirika la wanachama wote.
WITO KWA SERIKALI NA WADAU
Natoa wito kwa Serikali, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, wataalamu wa afya, watafiti, taasisi za elimu, Vyombo vya Habari na wadau wa mazingira kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza tiba asili, tafiti, elimu, usalama wa dawa, afya ya jamii na uhifadhi wa mazingira.
Tunaamini kuwa ushirikiano wa kitaalamu, heshima na mawasiliano ya wazi ndiyo njia bora ya kujenga sekta yenye manufaa kwa wananchi.
Tiba asili inahitaji maendeleo yanayozingatia maarifa ya jadi, sayansi, usalama, maadili na ushahidi.
UJUMBE WANGU KWA KILA MWANACHAMA
Katika Wiki hii ya Huduma, kila mmoja wetu ajiulize:
Ninamhudumia nani?
Ninamhudumia kwa moyo gani?
Huduma yangu inaleta faraja?
Inalinda afya?
Inalinda mazingira?
Na ninachangia nini katika kujenga Shirika letu?
Majibu ya maswali haya yawe chachu ya kuboresha huduma zetu na kuimarisha mshikamano wetu.
HITIMISHO
Kwa niaba ya Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania, ninawapongeza na kuwashukuru wote wanaotoa huduma kwa jamii kwa moyo wa kujitolea.
Tufanye Wiki ya Huduma kuwa zaidi ya maadhimisho ya siku chache. Iwe mwanzo wa utamaduni wa kudumu wa kuhudumia, kusaidiana, kuheshimiana, kulinda afya na kutunza mazingira.
“HUDUMA NI WAJIBU WETU, UPENDO NI MSINGI WETU, AFYA NA MAZINGIRA NI DHAMANA YETU.”
UMOJA WETU NDIO NGUVU YETU.
Boniventura Mwalongo
Katibu Mkuu, Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania & Mtaalamu wa Tiba Asili
Dar es Salaam, Tanzania



