Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Saaam
SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake kutoka Sh bilioni 1.3 hadi takribani Sh bilioni 147.8 katika mwaka wa fedha 2025/26, mafanikio yanayohusishwa na mageuzi ya kiutendaji, uwekezaji katika miradi ya madini na kuimarisha usimamizi.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. CPA Venance Mwasse, amesema mageuzi yaliyoanza mwaka 2020 yameimarisha uwezo wa shirika kujiendesha na kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali.
Amesema STAMICO, iliyoanzishwa mwaka 1972 na inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali, inashiriki katika mnyororo wa thamani wa madini kuanzia utafiti na uchimbaji hadi uchenjuaji, uongezaji thamani na biashara ya madini.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa watumishi kutoka 111 hadi karibu 800, kuingia mikataba minne ya ubia katika miradi ya madini ya kimkakati na kuendelea kuboresha mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Songwe.
Kuhusu wachimbaji wadogo, amesema shirika limeongeza mitambo ya uchorongaji kutoka mitatu hadi 18 na kuweka mitambo 17 kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji, sambamba na kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalamu.
Aidha, amesema STAMICO ina masoko 44 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini takribani 120, vinavyorahisisha uuzaji rasmi wa madini na kusaidia kupunguza utoroshaji.
Ameongeza kuwa mchakato wa kuanzisha Benki ya Wachimbaji Tanzania umeanza kwa kushirikiana na wadau, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wachimbaji wadogo.
Dkt. Mwasse amesisitiza kuwa STAMICO ni mwekezaji katika sekta ya madini, si mdhibiti, jukumu linalotekelezwa na taasisi husika za Serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema mafanikio ya STAMICO yanaonyesha umuhimu wa mageuzi katika taasisi za umma, huku akisisitiza haja ya kuimarisha utafiti na ukusanyaji wa takwimu za kisasa ili kupima matokeo ya shughuli zake kwa usahihi.




