Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
MKURUGENZI wa Manispaa ya Kibaha, Warda Abeid Maulid, amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kimkakati katika manispaa hiyo kuongeza kasi ya ujenzi ili ikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Maulid ametoa agizo hilo ,wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maeneo ya Misugusugu, Kongowe, Picha ya Ndege, Tangini na Tumbi.
Kadhalika ametembelea mradi wa maegesho ya malori, vituo vya kibiashara vya Kongowe na Kwa Mbonde, kituo cha biashara cha ATN kilichopo Picha ya Ndege, pamoja na miradi inayotekelezwa kupitia Mpango wa Uendelezaji Miji Tanzania (TACTIC), ikiwemo ujenzi wa barabara na Soko la Loliondo.
Akiwa katika Soko la Loliondo, Maulid amemtaka mkandarasi kuongeza juhudi na kutumia muda wa ziada inapowezekana ili kuharakisha ujenzi na kuhakikisha soko hilo linakamilika kwa wakati.
Amesisitiza kuwa kukamilika kwa soko hilo pamoja na barabara zinazojengwa kutaboresha mazingira ya biashara, kurahisisha shughuli za wafanyabiashara na kuwawezesha wananchi kupata huduma katika mazingira bora.
Aidha, amewataka wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha wakandarasi wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia masharti ya mikataba na muda uliopangwa, akieleza kuwa usimamizi madhubuti ni muhimu katika kuhakikisha miradi inakamilika na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi huyo pia ametembelea jengo la utawala la Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wake.
Miradi hiyo inalenga kuboresha miundombinu, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuongeza fursa za kiuchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Manispaa ya Kibaha.






