Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limeonya kuwa litafuta matokeo ya mtahiniwa yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu katika Mtihani wa Kidato cha Nne wa mwaka 2026, unaotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 6 mwaka huu.

Onyo hilo limetolewa Oktoba 18, 2026, na Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Ally Mohammed, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mtihani huo, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokiuka kanuni na taratibu za mitihani.

Profesa Mohammed amesema maandalizi ya mtihani huo yamekamilika, yakiwemo usambazaji wa karatasi za mitihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka nyingine muhimu katika halmashauri na manispaa zote za Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zimekamilisha maandalizi ya vituo, kutoa mafunzo kwa wasimamizi na kuweka mikakati ya kudhibiti mianya inayoweza kusababisha udanganyifu.

Aidha, amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa kuimarisha usalama wa vituo ili kuhakikisha watahiniwa wanafanya mitihani yao katika mazingira ya utulivu na kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa.

Amesisitiza kuwa wasimamizi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa umakini, uadilifu na weledi, huku wakihakikisha kila mtahiniwa anapata haki yake na kufanya mtihani ndani ya muda uliopangwa.

Kwa mujibu wa NECTA, watahiniwa wenye mahitaji maalumu wanapaswa kupatiwa mazingira rafiki yatakayowawezesha kufanya mtihani kwa usawa na watahiniwa wengine.

Amesema hatua hizo ni pamoja na kutoa maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa wenye uoni hafifu.

Vilevile, watahiniwa hao wanapaswa kuongezewa muda wa dakika 20 kwa kila saa katika somo la Hisabati ya Msingi na dakika 10 kwa kila saa katika masomo mengine, kwa mujibu wa mwongozo wa Baraza hilo.

NECTA imewataka wamiliki wa shule kutokuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani, huku wakuu wa shule wakisisitizwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Baraza hilo na kuepuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa ndani ya vyumba vya mitihani.

Katika hatua nyingine, Baraza hilo limeonya kuwa litafuta kituo chochote cha mtihani endapo litathibitisha kuwepo kwa matukio au vitendo vinavyohatarisha usalama na uadilifu wa mtihani.

NECTA pia imezitaka jamii na wananchi kuhakikisha watu wasiohusika hawaingii katika maeneo ya shule yanayotumika kama vituo vya mitihani katika kipindi chote cha mtihani, ili kulinda utulivu na kuwapa watahiniwa nafasi ya kufanya mitihani yao bila usumbufu.

Akizungumzia umuhimu wa mtihani huo, Profesa Mohammed amesema Mtihani wa Kidato cha Nne hupima umahiri wa wanafunzi katika masomo waliyosoma kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne.

Amesema matokeo yake hutumika pia katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano na kozi mbalimbali za kitaaluma, zikiwemo za afya, kilimo na ufundi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na NECTA, jumla ya watahiniwa 667,040 wamesajiliwa kufanya mtihani huo mwaka huu, wakiwemo watahiniwa wa shule 664,085 na watahiniwa wa kujitegemea 22,955.

Aidha, takwimu hizo zinaonesha kuwa wavulana ni 297,309, sawa na asilimia 46.16, huku wasichana wakiwa 297,776, sawa na asilimia 53.84. Jumla ya watahiniwa 910 wa shule wanahitaji huduma maalumu.

Katika kuhakikisha mtihani unafanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni, NECTA imewataka wananchi wanaobaini vitendo vya udanganyifu kutoa taarifa kupitia namba ya simu 0759360000 au barua pepe [email protected].

Baraza hilo limesema litafanyia kazi taarifa zitakazowasilishwa na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.