Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
JUMLA ya watahiniwa 667,040 wamesajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu, huku Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) likitoa wito kwa wadau wa elimu kuhakikisha mtihani huo unafanyika kwa amani, utulivu na kuzingatia kanuni, licha ya changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua katika baadhi ya maeneo nchini.
Mtihani huo utafanyika kuanzia kesho Oktoba 19 hadi Novemba 6, 2026, katika shule za sekondari 6,265 na vituo 802 vya watahiniwa wa kujitegemea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 18, 2026 jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, amesema kati ya watahiniwa waliosajiliwa, 644,085 ni wa shule na 22,955 ni wa kujitegemea.
Amesema kati ya watahiniwa wa shule, wavulana ni 297,309 sawa na asilimia 46.16, huku wasichana wakiwa 346,776 sawa na asilimia 53.84.
Aidha, watahiniwa wa shule wenye mahitaji maalum ni 910, wakiwemo wenye uoni hafifu 455, wasioona 13, wenye uziwi 98, wenye ulemavu wa akili 21 na wenye ulemavu wa viungo 323.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea amesema wavulana ni 10,223 sawa na asilimia 44.53, huku wasichana wakiwa 12,732 sawa na asilimia 55.47. Watahiniwa 73 wa kundi hilo wana mahitaji maalum, wakiwemo wenye uoni hafifu 69 na wasioona wanne.
Profesa Mohamed amesema idadi ya watahiniwa wa shule imeongezeka kutoka 569,883 mwaka 2025 hadi 644,085 mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la watahiniwa 74,202 sawa na asilimia 13.02.
Amesema mtihani huo ni muhimu kwa kuwa unapima umahiri wa watahiniwa katika masomo waliyosoma kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne, huku matokeo yake yakitumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano na mafunzo mbalimbali ya kitaalamu, yakiwemo ya afya, kilimo na ufundi.
Kuhusu athari za mvua, amesema NECTA imebadilisha ratiba za mitihani na kuyaelekeza kamati za mitihani kuchukua hatua stahiki katika maeneo yatakayoathiriwa ili kuhakikisha watahiniwa wanapata nafasi ya kufanya mitihani yao.
Amesema mtahiniwa atakayeshindwa kabisa kufanya mtihani kutokana na athari hizo hatapoteza haki yake, kwani atapewa nafasi ya kufanya mtihani katika awamu inayofuata.
NECTA imezitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha usalama wa vituo vya mitihani unaimarishwa na vituo vinatumika kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Baraza hilo.
Pia, wasimamizi wa mitihani wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa umakini, uadilifu na weledi ili kuhakikisha kila mtahiniwa anapata haki yake na kufanya mtihani kwa muda uliopangwa katika mazingira ya utulivu.
Akizungumzia watahiniwa wenye mahitaji maalum, Profesa Mohamed amesisitiza kuwa wanapaswa kupatiwa huduma zinazostahili, ikiwemo karatasi za mtihani zilizoandikwa kwa nukta nundu kwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa wenye uoni hafifu.
Amesema watahiniwa hao pia wanapaswa kuongezewa dakika 20 kwa kila saa katika somo la Basic Mathematics na dakika 10 kwa kila saa katika masomo mengine, kwa mujibu wa mwongozo wa Baraza.
NECTA imesema inatarajia watahiniwa wa shule na wa kujitegemea watafanya mitihani hiyo kwa kuzingatia kanuni, huku ikionya kuwa mtahiniwa yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu atafutiwa matokeo yake kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Vilevile, wamiliki wa shule wametakiwa kutokuingilia majukumu ya wasimamizi wakati wote wa mtihani, huku wakuu wa shule wakitakiwa kuzingatia miongozo ya usimamizi na kuepuka kuingilia shughuli za usimamizi ndani ya vyumba vya mitihani.
Baraza limeonya kuwa halitasita kufuta kituo chochote cha mtihani litakapojiridhisha kuwa kuna matukio au vitendo vinavyohatarisha usalama wa mtihani.
Aidha, wananchi wametakiwa kuhakikisha maeneo ya shule yanakuwa salama na watu wasiohusika hawaingii katika maeneo hayo wakati wa mitihani. Wadau wa elimu na wananchi pia wametakiwa kushirikiana na mamlaka husika kudhibiti udanganyifu na kutoa taarifa wanapobaini vitendo hivyo.


