Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imemtuhumu rais wa zamani wa taifa hilo, Joseph Kabila,kwa kujaribu kuipindua serikali ya sasa ili kurejea madarakani.
Waziri wa Habari wa DRC, Patrick Muyaya, ambaye pia ni msemaji wa serikali, amesema uamuzi wa Kabila kutumia nguvu na silaha unaashiria nia yake ya kutaka kuwaangamiza raia wa DRC na kukiuka katiba.
Katika taarifa yake kuhusu vuguvugu jipya la waasi linalohusishwa na Kabila, Muyaya amesema kuwa “ingawa kundi hilo linajaribu kubadilisha sura yake, nia yake, mipango yake na mbinu zake zinafahamika.”
Waziri huyo amedai kuwa kundi hilo ni muungano wa waasi wanaoshirikiana na Rwanda, tuhuma ambazo hazijathibitishwa.
Muyaya amesema serikali ya DRC bado imejitolea kutafuta suluhu ya mzozo wa usalama unaoikumba taifa hilo,kupitia michakato ya kidiplomasia ya Washington na Doha.

