KINSHASA, DRC

Wiki iliyopita kumeibuka taarifa za kushangaza kwa Waafrika na baadhi ya wachambuzi wa siasa za kimataifa baada ya Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila, kuungana na waasi wa AFC/M23 na kuunda muungano wa Front pour Refondation de la Nation (FRN).

Kwa sasa Kabila ndie Rais wa muungano huo mpya unaotajwa kuwa wa kisiasa na kijeshi na utaunganisha nguvu, rasilimali na uwezo wake ili kumaliza kile unachodai ni utawala wa mabavu kwa kutumia njia zote.

Katika nafasi yake, atasaidiwa na makamu wake kutoka M23 na hayo ni mabadiliko makubwa zaidi katika uongozi wa uasi huo kwa miaka ya karibuni.

Hatua hiyo inawapa waasi kiongozi maarufu wa DRC anayeweza kuwasaidia kujionyesha kama vuguvugu la kitaifa. Kwa mujibu wa wanadiplomasia, vyanzo vya waasi na wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema uteuzi huo unaweza pia kusaidia kupunguza taswira ya kundi hilo kuwa chombo cha kutekeleza maslahi ya Rwanda.

Hata hivyo, jina kubwa pekee halitoshi kubadili hali ya kisiasa au kijeshi. Swali kuu ni iwapo ataweza kutumia uzoefu, uhusiano na ushawishi aliobakiwa nao kuvutia wafuasi wapya ndani na nje ya DRC?

Licha ya kujiunga, sehemu kubwa ya uongozi wa zamani imebaki.

Corneille Nangaa na Bertrand Bisimwa wamekuwa Makamu wa Rais huku Sultani Makenga akipewa nafasi hiyo na kuendelea kuongoza upande wa kijeshi.

Historia inampa Kabila uzito wa kisiasa na umaarufu mkubwa zaidi kuliko viongozi wengi waliouongoza muungano huo.

Anatoka eneo la Katanga lililopo kusini mwa nchi hiyo ambako kuna ongezeko la kutoridhishwa na utawala wa Rais Felix Tshisekedi.

KWA HABARI KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 20 – 26, 2026