• Hifadhi ya Barabara ya Morogoro yajengwa vituo vya mafuta, baa, kumbi za disko, fremu za maduka

• TANROADS yakiri kutoa vibali vya mwaka mmoja, yashangazwa na ujenzi ‘wa kudumu’

• Wananchi wakumbuka ubomoaji wa nyumba, wahoji usawa mbele ya sheria

Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Matajiri wenye ukwasi, ‘wamegawana’ maeneo ya hifadhi ya barabara kuanzia Kimara jijini Dar es Salaam hadi Maili Moja, Kibaha mkoani Pwani.

Ujenzi unaoendelea kwa kasi eneo hilo ni wa vituo vya mafuta, baa, kumbi za starehe, fremu za maduka na maegesho ya malori.

Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, ameulizwa na JAMHURI kuhusu kadhia hii, na amesema: “Sina taarifa kabisa za ujenzi huo, naomba muda nifuatulie na nitatoa taarifa.”

Kadogosa aliteuliwa kushika wadhifa huo kutoka kwa Abdallah Ulega Septemba 27, mwaka huu,, na kukabidhiwa ofisi Oktoba 2, mwaka huu.

Hifadhi hii ya Barabara ya Morogoro, ni hifadhi kubwa kwa upana kuliko hifadhi za barabara nchini, ikiwa imewekwa na wakoloni wa Kiingereza tangu mwaka 1932.

Ni hifadhi hii ya barabara ambayo mwaka 2017/2018 Rais Dk. John Magufuli, kwa mamlaka aliyokuwa nayo, aliamuru kuvunjwa kwa mamia ya nyumba za wananchi waliojenga ndani ya hifadhi.

Katika ubomoaji huo, wananchi hawakulipwa fidia. Katika eneo kama la Luguruni, Kata ya Kwembe, bado kunaonekana makaburi mengi ya familia zilizojenga na kuishi ndani ya hifadhi kwa miongo mingi.

Wakati vilio vya wananchi walioondolewa vikiwa vibichi, mamlaka zimewapa ruhusa baadhi ya watu wenye ukwasi kujenga huduma mbalimbali kwa misingi ya kukodi.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na JAMHURI wanahoji kwa nini maeneo yaliyopigwa marufuku kwa makazi na biashara yanatumiwa na wawekezaji, baadhi yao wakijenga vitega uchumi vya kudumu.

Mmoja wa wataalamu wa ujenzi wa vituo vya mafuta amesema kwa mwonekano, baadhi ya vituo vilivyojengwa thamani yake inakaribia au hata kupita Sh bilioni 1.

“Huwezi kusema ujenzi huu ni ‘temporary’ ilhali unaona uwekezaji mkubwa wa mamilioni kwa mabilioni ya shilingi. Ninavyojua, sheria ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) anatoa vibali kwa ujenzi wa vitu vya dharura, siyo uwekezaji wa haya mamilioni,” anasema.

JAMHURI imeshuhudia kwa miezi ya karibuni ujenzi ukiwa umepamba moto katika maeneo ya Kimara Stop Over, Suka, Temboni, Kibanda cha Mkaa, Kwa Yusuf, Luguruni, Kibamba Hospitali, Kibamba CCM, Kibamba Shule, Kwa Komba na Kiluvya.

Katika eneo la Kibanda cha Mkaa, upande wa kushoto (kwa uelekeo wa Kibaha), kumejengwa jumba la starehe linalohusisha baa ya vinywaji, na taarifa zilizopo ni kwamba uzinduzi utafanywa wakati wowote kuanzia sasa.

Katika eneo la Temboni, kunajengwa vituo vitatu vya mafuta, huku kukiwa na kuta ndefu zilizosheheni vyumba ambavyo kwa mwonekano wa kawaida ni fremu za maduka ya biashara.

Ujenzi huu unafanywa bila kujali vituo vya mafuta vilivyo jirani vilivyojengwa nje ya hifadhi ya barabara kwa kutii agizo na mamlaka ya Serikali.

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 20- 26, 2026