*Ripoti ya TIRA ya mwaka 2025 yaonyesha soko la bima Tanzania kukua hadi Sh trilioni 2.55 kutoka Sh trilioni 1.52
*Watu milioni 26.8 wanafikiwa na huduma za bima, lakini mchango wa bima katika Pato la Taifa ni asilimia 2.11 tu
*TIRA yabainisha changamoto za udanganyifu, huduma chache vijijini na uwezo mdogo wa kampuni za ndani kukabili hatari za uwekezaji
NA Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Soko la bima Tanzania limepata ukuaji mkubwa wa biashara, lakini ongezeko hilo linaibua maswali kuhusu kasi ya upanuzi wa huduma, uwezo wa kampuni kulipa madai na kiwango ambacho wananchi wananufaika na mfumo wa bima.
Ripoti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), inayohusu utendaji wa soko kwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2025, inaonyesha kuwa thamani ya jumla ya biashara ya bima ilifikia Sh trilioni 2.55, kutoka Sh trilioni 1.52 mwaka 2024. Hilo ni ongezeko la asilimia 68.4.
Katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi za TIRA, Njedengwa, jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Ali Munde, alizindua ripoti hiyo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba.
Takwimu nyingine ndani ya ripoti hiyo zinaonyesha kuwa, pamoja na kukua kwa biashara, bado kuna changamoto za upatikanaji wa huduma, ulipaji wa madai, udanganyifu na uwezo wa kampuni za ndani kukabili hatari kubwa za kiuchumi.
Ripoti hiyo, iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dodoma, inatoa picha ya sekta inayopanuka kwa kasi, lakini ambayo bado inakabiliwa na kazi ya kuhakikisha ukuaji wa mapato unaambatana na ulinzi madhubuti wa wateja na upanuzi wa huduma kwa wananchi wengi zaidi.
Miongoni mwa takwimu zinazotazamwa kwa karibu ni ongezeko la madai ya bima yaliyoripotiwa katika kipindi hicho.
Kwa mujibu wa Kamishna wa TIRA, Dk. Bughayo Saqware, madai yote yaliyoripotiwa mwaka 2025 yalifikia Sh trilioni 1.61, kutoka Sh bilioni 727.7 mwaka uliotangulia. Hilo ni ongezeko la asilimia 120.8.
Kati ya madai hayo, kampuni za bima zililipa Sh trilioni 1.29, sawa na asilimia 80.25 ya thamani ya madai yaliyoripotiwa. Sh bilioni 317.37 zilizobaki zilikuwa katika hatua mbalimbali za uchakataji, ikiwamo uhakiki wa uhalali wa madai na nyaraka zinazohitajika.
Hii ina maana kwamba, hadi mwisho wa kipindi kilichoripotiwa, kiasi kikubwa cha fedha kilikuwa bado hakijalipwa kwa sababu mbalimbali za kiutendaji na kiuhakiki.
KWA HABARI ZAIDI ZA KINA SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 20 – 26, 2026


