• Mapato yapaa kutoka Sh bilioni 1.3 hadi bilioni 147.8, Dk. Mwasse aongoza mageuzi

• Yakuza wachimbaji wadogo, wachangia asilimia 40; yaongeza wafanyakazi kutoka 205 hadi 872

• Kiwira iliyokuwa sikio la kufa yaigeuza mgodi wenye faida, wananchi wanufaika

Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KUNA wakati katika maisha ya taifa tunalazimika kujiuliza maswali magumu. Je, mashirika yetu ya umma yanaweza kujiendesha kwa faida? Je, Serikali inaweza kufanya biashara kwa ufanisi bila kutegemea ruzuku kila mwaka? Je, rasilimali za madini tulizojaliwa na Mwenyezi Mungu zinaweza kuwanufaisha Watanzania wengi badala ya wachache?

Maswali haya yamekuwa yakijadiliwa kwa miaka mingi. Wapo wanaoamini kuwa Serikali haiwezi kufanya biashara kwa ufanisi, na wapo wanaosisitiza kuwa tatizo si umiliki wa Serikali, bali namna mashirika hayo yanavyoongozwa, kusimamiwa na kuwajibishwa.

Oktoba 16, 2026, nilipata fursa ya kusikiliza wasilisho la Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), lililotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Dk. CPA Venance Mwasse, jijini Dar es Salaam, alipokutana na wahariri.

Niseme wazi kuwa nilichokisikia kimenifanya nitafakari upya uwezo wa mashirika yetu ya umma. Takwimu, miradi, mikakati na mabadiliko ya kiutendaji yaliyowasilishwa yanatoa somo kubwa kwa Watanzania, viongozi wa taasisi za umma na hata sekta binafsi. Ndiyo maana nimeamua kuandika makala hii nikisema STAMICO imetufumbua macho Watanzania.

Hili si suala la kusifia taasisi kwa sababu tu imewasilisha takwimu nzuri. Ni suala la kuchunguza namna shirika lililopitia misukosuko mikubwa linavyoweza kujipanga upya, kuongeza mapato, kuwekeza katika uzalishaji, kutoa ajira na kushiriki katika kujenga uchumi wa taifa.

STAMICO ilianzishwa mwaka 1972 ikiwa inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania. Lengo lake lilikuwa kuhakikisha taifa linashiriki kikamilifu katika shughuli za utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani na biashara ya madini.

Falsafa iliyosababisha kuanzishwa kwake ilikuwa rahisi, lakini yenye maana kubwa kwamba madini ni rasilimali zinazokwisha. Yakishachimbwa na kuuzwa, hayawezi kurudishwa ardhini. Kwa hiyo, taifa lazima lihakikishe linapata manufaa yanayostahili wakati rasilimali hizo zikiendelea kuvunwa.

Hata hivyo, kuwa na rasilimali nyingi hakumaanishi moja kwa moja kuwa na uchumi imara. Kinachotengeneza utajiri ni uwezo wa kuzisimamia, kuwekeza, kuongeza thamani na kuhakikisha mapato yanayopatikana yanawanufaisha wananchi.

Katika historia yake, STAMICO imepitia vipindi vya mafanikio na changamoto. Ilifikia wakati ambapo maswali yaliibuka kuhusu uwezo wake wa kuendelea kuwepo kama shirika lenye tija kwa taifa.

Lakini kile kinachoonekana sasa ni juhudi za kuondoka katika historia hiyo na kujenga shirika linalofanya biashara, kuwekeza katika miradi yenye tija na kupima mafanikio kwa matokeo.

Safari hiyo imejengwa katika mabadiliko ya uongozi, utamaduni wa uwajibikaji, upangaji upya wa miradi, ushirikishwaji wa wafanyakazi na wadau, pamoja na matumizi ya viashiria vya kupima utendaji.

Hapa ndipo somo la kwanza linapopatikana. Shirika la umma halipaswi kupimwa kwa ukubwa wa ofisi zake, idadi ya magari ya viongozi au wingi wa mikutano. Linapaswa kupimwa kwa thamani inayozalishwa, mapato yanayopatikana, ajira zinazotengenezwa na mchango wake kwa maendeleo ya wananchi.

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 20 -26, 2026