Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Baadhi ya madereva waliofungiwa leseni kutokana na kukatwa pointi kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani wamelalamikia kuchelewa kurejeshewa leseni zao, licha ya kuhudhuria mafunzo na kufanya mitihani iliyoandaliwa na mamlaka husika.
Madereva hao wamesema wamekamilisha hatua za mafunzo na mitihani kama walivyoelekezwa na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, lakini baadhi yao hawajarejeshewa leseni, hali inayowalazimu kutafuta shughuli nyingine za kujipatia kipato.
Mmoja wao, Daudi Joseph, amesema alihudhuria mafunzo na kufanya mtihani katika Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani, Dar es Salaam, baada ya leseni yake kufungiwa kutokana na mfumo wa pointi.
Amesema siku ya mtihani walipewa maswali 35 kuhusu usalama barabarani, yaliyolenga kupima uelewa wao na kuwasaidia kuboresha mwenendo wanapotumia barabara.
“Nilikwenda kufanya mtihani pamoja na wenzangu 41. Tulifanya kama sehemu ya utaratibu wa kurejeshewa leseni zetu na madaraja tuliyokuwa nayo.
“Tulielezwa kwamba baada ya hatua hiyo tungerejeshewa leseni, lakini hadi sasa sijapewa yangu. Siku hiyo tulifaulu,” amesema.
Amesema kabla ya kufanya mtihani, madereva waliwasilisha barua za kuomba msamaha baada ya leseni zao kufungiwa, ndipo walipopata nafasi ya kuhudhuria mafunzo na kufanya mitihani.
Maisha bila leseni
Joseph amesema kukosa leseni kumemwathiri kiuchumi kwa sababu udereva ndiyo kazi aliyokuwa akiitegemea kuendesha maisha yake na familia.


