Wizara ya Nishati imetoa elimu kuhusu Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, katika mkutano uliofanyika Oktoba 22, 2026, jijini Mbeya.

Akitoa mafunzo hayo, Mhandisi Benezeth Kabunduguru kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Wizara ya Nishati, amesema jumla ya taasisi 2,682 zimeanza kutumia nishati safi ya kupikia kati ya taasisi 30,000 zinazolengwa na Serikali.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mei 8, 2024.

Mhandisi Kabunduguru ameeleza kuwa matumizi ya kuni na mkaa yanaweza kusababisha athari za kiafya kutokana na moshi unaozalishwa wakati wa kupikia, sambamba na kuchangia uharibifu wa misitu na mazingira. Amebainisha kuwa nishati safi za kupikia ni pamoja na umeme, gesi oevu (LPG), gesi asilia, gesi vunde, bayoethanoli, mkaa mbadala, nishati ya jua na hidrojeni.

Aidha, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yana manufaa ya kiafya, kimazingira na kiuchumi, ikiwemo kupunguza muda unaotumika kutafuta kuni, kuhifadhi misitu na kuwawezesha wanawake na watoto kutumia muda mwingi katika shughuli za uzalishaji na masomo.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza hatua mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, zikiwemo kusambaza majiko na mitungi ya gesi kwa ruzuku, kuimarisha miundombinu ya gesi asilia na kuhamasisha matumizi ya majiko ya umeme.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100 kwa siku kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia. Amewataka viongozi na watumishi wa umma kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati hiyo katika maeneo yao ya kazi na jamii zinazowazunguka ili kuchangia kufanikisha lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Kwa upande wake, Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi, ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kutoa mafunzo hayo, akieleza kuwa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ni muhimu katika kuongeza uelewa na kuhamasisha mabadiliko ya matumizi ya nishati katika taasisi na jamii.