Na Mwandishi Wetu, Jamuhuri Media, Songea.
Waziri wa Nishati, Juma Homera, amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linakamilisha mkataba wa kupeleka umeme katika mradi wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kutengeneza aluminium kinachojengwa eneo la Mwenge Mshindo, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.
Homera amesisitiza umuhimu wa TANESCO kukamilisha taratibu za utiaji sahihi mkataba huo hadi ifikapo Novemba mwaka huu wawe wameshakamilisha taratibu zote ili kuhakikisha mradi huo unapata huduma ya umeme inayohitajika kwa ajili ya kuendesha shughuli za uzalishaji mara baada ya kiwanda hicho kukamilika.
Akizungumza Leo alipotembelea mradi huo ambao unajengwa na Kampuni ya Hongwang Tanzania Holding Limited (HWTZ) katika eneo la viwanda lililopo mwengemshindo Manispaa ya Songea, amesema kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika ni miongoni mwa mahitaji muhimu katika kuhakikisha uwekezaji wa kiwanda hicho unafanikiwa.
Aidha, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kwamba changamoto zinazoweza kuchelewesha upatikanaji wa umeme zinapatiwa ufumbuzi mapema kupitia ushirikiano kati ya TANESCO na wawekezaji.
Kiwanda hicho kinachojengwa Mwenge Mshindo, Manispaa ya Songea, kinatarajiwa kuwa sehemu ya shughuli za uwekezaji wa viwanda mkoani Ruvuma, huku kukamilika kwake kukitegemea pia upatikanaji wa miundombinu muhimu, ikiwemo umeme, barabara pamoja na ajira kwa wazawa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahamed Habasi amesema kuwa mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi Trioni 7.8 na ukikamilika unatarajia utatoa ajira kwa watu zaidi ya 5000.




