WAHITIMU wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya, wametakiwa kutumia elimu na ujuzi walioupata chuoni kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kuzingatia utu, uadilifu na maadili ya Kitanzania, huku wakitumia ubunifu na uthubutu kutafuta suluhisho la changamoto zinazowazunguka.
Wito huo umetolewa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, wakati wa Mahafali ya 25 ya chuo hicho yaliyofanyika tarehe 26 Oktoba 2026, katika Ndaki ya Mbeya, mkoani Mbeya.
Mheshimiwa Dkt. Shein amewasisitiza wahitimu hao kutumia maarifa na ujuzi walioupata kwa manufaa ya jamii, akieleza umuhimu wa kujitofautisha kupitia matendo yanayoonesha utu, uadilifu, kuheshimu wengine na kuzingatia maadili ya Kitanzania. Amesisitiza kuwa elimu inapaswa kuwa nyenzo ya kuboresha maisha ya watu na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Mlau wa Mahafali, Prof. Elizabeth Lulu Genda, amewataka wahitimu kukabiliana na changamoto za maisha kwa uvumilivu, ubunifu na uthubutu badala ya kulaumu Serikali, mifumo au jamii wanapokutana na vikwazo.
Prof. Genda amesema ukosefu wa ajira, mitaji, urasimu na uhaba wa fursa ni miongoni mwa changamoto ambazo wahitimu wanaweza kukutana nazo wanaporejea katika jamii, hivyo wanapaswa kutafuta mbinu sahihi za kuzivuka badala ya kukata tamaa.
“Msipoteze muda na rasilimali zenu kugombana na mambo yatakayowakinga katika safari ya maisha. Chunguzeni kwa makini na kutafuta namna ya kuvuka vikwazo hivyo,” alisisitiza Prof. Genda.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amewataka wahitimu kutumia elimu yao kwa uadilifu, ubunifu na bidii ili kuanzisha shughuli za uzalishaji mali, kutengeneza fursa na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Prof. Mwegoha pia amewahimiza wahitimu kudumisha uhusiano na chuo chao kwa kushirikiana, kushauriana na kusaidia wanafunzi kupata fursa za ajira na ujasiriamali, akisisitiza kuwa mtandao wa wahitimu unaweza kuunganisha maarifa, uzoefu na fursa kwa manufaa ya wahitimu wenyewe, chuo na jamii kwa ujumla.
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 1,212, wakiwemo wanaume 587 na wanawake 625, wametunukiwa tuzo za kitaaluma katika ngazi za Shahada ya Umahiri, Shahada ya Awali, Stashahada na Astashahada.
Naye, mhitimu bora wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Ndg. Lugano Mwapongo amewataka wahitimu kutumia maarifa waliopata chuoni hapo kuleta maendeleo katika jamii. Aidha, ameeleza kuwa ni mwiko kukata tamaa hivyo wahitimu na wanafunzi waendelee kuweka juhudi zenye kuleta mafanikio.
Mahafali hayo yanaweka bayana kuwa thamani ya elimu haipo katika vyeti pekee, bali pia katika uwezo wa wahitimu kutumia maarifa yao kutatua changamoto, kufungua fursa na kuboresha maisha ya watu. Kwa wahitimu hao, hatua inayofuata ni kuyageuza maarifa waliyoyapata chuoni kuwa matokeo yanayoonekana katika jamii na maendeleo ya Taifa.




