Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Oktoba 31, 2026
MRATIBU wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid), Wakili Innocent Magesa, amesema mwamko wa wananchi katika siku tatu za awali za kampeni hiyo ni mzuri, huku akiwataka kuendelea kujitokeza kupata huduma za kisheria na utatuzi wa migogoro katika halmashauri zote za Mkoa wa Pwani.
Akitoa taarifa kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Richard Kayombo, alipotembelea mabanda ya maonyesho ya kampeni hiyo yaliyopo Maili Moja, Manispaa ya Kibaha, Magesa amesema awamu ya pili ya kampeni hiyo inatekelezwa kwa siku 10, kuanzia Oktoba 28 hadi Novemba 7, mwaka huu.
Ameeleza pamoja na mwitikio kuwa mzuri, bado wananchi wana siku saba za kupata huduma hizo, hivyo wanapaswa kutumia fursa hiyo kujitokeza na kuwasilisha changamoto zao.
“Mwitikio ni mzuri kiasi hiki, na hii ni kutokana na kwamba bado tuna siku saba mbele, Wananchi watumie fursa hii ili waweze kunufaika,” ameelezea Magesa.
Kwa upande wake, Kayombo amesema amefurahishwa na mwitikio wa wananchi na kuwataka wenye migogoro ya ardhi, ndoa na mirathi, pamoja na wanaohitaji huduma za usuluhishi na msaada kutoka TAKUKURU, kufika katika mabanda hayo kupata elimu na mwongozo wa kisheria.
Ameelezea Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa maeneo yenye migogoro mingi ya ardhi, huku baadhi ya wananchi wakiingia katika migogoro hiyo kutokana na kasoro zinazojitokeza katika hatua za awali za mauziano ya ardhi, hivyo elimu ya kisheria ni muhimu katika kuzuia changamoto hizo.
Mkazi wa Mwanalugali, Ally Maandiko, amesema amepata msaada wa kisheria kuhusu kero ya mgogoro wa ardhi unaomkabili, ambapo wataalamu wamemwelekeza hatua za kuchukua pamoja na namna ya kufuatilia suala lake.
Ally ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea wananchi huduma za msaada wa kisheria zinazowasaidia kutatua kero zao bila malipo wala vikwazo.
Naye Ofisa Mahusiano wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Anneth Mwakatobe, amesema taasisi hiyo imekuwa ikipokea mashauri mbalimbali kutoka kwa wananchi, huku migogoro ya ardhi ikitajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa.
Amebainisha TAKUKURU imejipanga kuanza ziara za kata kwa kata kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi na kukabiliana na migogoro ya ardhi inayohusisha vitendo vya rushwa.







