*Ni kwa ajili ya mtaji, mitambo na CIP

*Atoa leseni kwa vikundi 118 kupitia Mradi wa MBT, ataka mitaji itumike kuongeza uzalishaji

*Rais Samia apongezwa kukuza Sekta ya Madini

SONGWE
NA MWANDISHI WETU

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameshuhudia makabidhiano ya mkopo wa Sh bilioni 50 kutoka Benki ya CRDB kwenda kwa kikundi cha wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu cha Songwe Gold Family (SGF) kwa lengo la kuongeza mitaji, uzalishaji na tija katika shughuli za uchimbaji.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mavunde, amewataka wachimbaji kutumia mkopo huo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza uzalishaji na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.

Amesema serikali itaendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mitaji, leseni na taarifa za kijiolojia zitakazowasaidia kufanya uchimbaji wenye tija.

Aidha, amempongeza Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo ya kuwezesha maeneo yenye leseni zilizorejeshwa serikalini kutolewa kwa wachimbaji wadogo huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya leseni zisizoendelezwa ili kutoa fursa kwa vikundi vyenye nia ya kufanya shughuli za uchimbaji.

Katika hatua nyingine, amekabidhi leseni za uchimbaji mdogo wa dhahabu kwa vikundi 81 kupitia Mradi wa Mining for a Brighter Tomorrow (MBT), unaolenga kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki katika mnyororo wa thamani wa madini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Matawi na Wateja Wadogo na Wakati wa CRDB, Bonventure Poul, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Madini kuwawezesha wachimbaji wadogo, wachakataji na wafanyabiashara wa madini kupata mitaji.

Amesema kati ya mikopo ya kiasi cha Sh bilioni 426 iliyotolewa na benki hiyo, Sh bilioni 150 zimeelekezwa kwa wachimbaji wadogo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Abubakar Kunenge, amesema serikali itaendelea kuunga mkono wachimbaji wadogo kwa kutambua mchango wao katika kukuza uchumi wa mkoa na Taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Dickson Nickson, ameitaja changamoto ya umeme kuwa kikwazo kwa wachimbaji na kuiomba serikali kuharakisha upatikanaji wa nishati hiyo katika maeneo ya uchimbaji.

Naye, Mbunge wa Songwe (CCM), Philip Mlugo, ameipongeza serikali kwa kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuzitaka benki nyingine kuiga mfano wa CRDB katika utoaji wa mikopo kwa sekta hiyo.