Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha Novemba 4, 2026
WANANCHI wametakiwa kuandika wosia mapema wakielezwa kuwa kufanya hivyo si kujichulia kifo, bali ni hatua muhimu ya kuweka wazi matakwa ya mmiliki wa mali na kujikinga na migogoro ya kifamilia inayoweza kujitokeza baada ya kifo chake.
Aidha, wananchi wameshauriwa kuhakikisha wosia una mashahidi wanaotakiwa kisheria na nyaraka hizo zinahifadhiwa mahali salama ili ziweze kupatikana na kutumika kwa wakati unaofaa, hatua itakayosaidia kupunguza chuki, migawanyiko na migogoro miongoni mwa warithi.
Wito huo umetolewa Novemba 4, 2026 na wataalamu wa masuala ya kisheria wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid), Manispaa ya Kibaha, wakati wakitoa elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria kwa wananchi wa Kata za Tumbi na Sofu.
Timu hiyo inayoongozwa na Wakili Revocatus Thadeo Mathew, imetoa elimu kuhusu umuhimu wa kuandika wosia, taratibu za mirathi na namna ya kulinda haki za warithi, huku ikisisitiza kuwa wosia unapaswa kuandaliwa kwa kuzingatia matakwa ya mmiliki wa mali na taratibu za kisheria.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Tumbi, Revocatus amesema kuandika wosia mapema kunasaidia kuondoa utata kuhusu mgawanyo wa mali na kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza baina ya wanafamilia baada ya mmiliki wa mali kufariki.
Katika kampeni hiyo, wananchi wa Kata za Tumbi na Sofu pia wamepatiwa elimu kuhusu masuala ya ardhi, ndoa na mirathi, huku wakipewa fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili na kupata ufafanuzi pamoja na ushauri wa kisheria kutoka kwa wataalamu hao.
Sambamba na hilo, elimu imetolewa kuhusu nafasi na majukumu ya Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata katika kusaidia kutatua migogoro inayojitokeza katika jamii, kwa kusisitiza umuhimu wa kutumia njia sahihi za kisheria katika kutafuta ufumbuzi.
Kadhalika, timu hiyo imetembelea shule za msingi na sekondari katika kata hizo na kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu ukatili wa kijinsia, namna ya kujitambua na kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili, pamoja na umuhimu wa kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo hivyo.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inaendelea katika kata mbalimbali za Manispaa ya Kibaha ikiwa na lengo la kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu haki na wajibu wao na kuwawezesha kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili kwa mujibu wa sheria.









