Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dares Salaam

BOLT imepanua huduma zake nchini kwa kuingia Iringa na Babati, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kufikisha huduma za usafiri wa kidijitali katika miji na maeneo yanayokua kiuchumi.

Bolt ilianza kutoa huduma Iringa Julai mwaka huu kabla ya kuingia Babati Oktoba 2026. Hatua hiyo imekuja wakati uchumi wa mikoa hiyo ukiendelea kukua. Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha kuwa mwaka 2025 uchumi wa Iringa ulikuwa na thamani ya takribani Sh trilioni 7.33, huku Manyara ukifikia Sh trilioni 7.83.

Lakini kwa mkazi wa kawaida, faida ya huduma hiyo inaonekana zaidi katika safari za kila siku. Kwa mfanyakazi anayemaliza zamu usiku Babati, changamoto inaweza kuwa kufika nyumbani kutoka barabara kuu hadi maeneo ya makazi ambako miundombinu bado inaendelea kuboreshwa. Uwezo wa kuagiza usafiri kupitia simu unaweza kurahisisha safari hiyo ya mwisho na kuongeza uhakika wa kufika anakoelekea.

Babati pia inanufaika na ujenzi wa barabara na taa kupitia mradi wa TACTIC, hatua inayolenga kuongeza usalama na kuwezesha shughuli za biashara kuendelea kwa muda mrefu zaidi. Iringa, huduma hiyo inaweza kumsaidia mtalii anayewasili Uwanja wa Ndege wa Nduli akiwa na dhana kuwa usafiri mtandao unapatikana Dar es Salaam na miji mikubwa pekee. Iringa ni moja ya milango muhimu ya kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Idadi ya wageni katika ukanda wa utalii wa Kusini ilifikia zaidi ya 205,000 kati ya Julai 2025 na Aprili 2026.

“Kwetu ukuaji si kufungua miji mipya pekee, bali kuhakikisha teknolojia ya usafiri inakuwa na maana katika maisha ya watu,” alisema Dimmy Kanyankole, Meneja Mkuu wa Bolt Afrika Mashariki.

“Iwe ni mfanyakazi anayerejea nyumbani usiku, mfanyabiashara anayekwenda kwa mteja au mtalii anayezuru Iringa, usafiri unapaswa kuwasaidia watu kufikia fursa za kiuchumi kwa urahisi zaidi.”

Babati pia ipo katika ukanda muhimu wa utalii, huku Lango jipya la Mamire la Hifadhi ya Taifa ya Tarangire likitarajiwa kuongeza mzunguko wa wageni kupitia eneo hilo. Hifadhi hiyo hupokea takribani watalii 372,000 kwa mwaka. Kwa Bolt, hoja ni moja: fursa za kiuchumi hazipaswi kuishia barabara kuu.

Usafiri wa safari za mwisho unaweza kuunganisha vituo vya mabasi, viwanja vya ndege na maeneo ya biashara na makazi, hoteli, masoko pamoja na maeneo ya utalii.