Ubalozi wa Tanzania nchini Canada umeshiriki Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii na Safari (SITV) ya Mwaka 2026 yaliyofanyika katika Mji wa Montreal.
Kupitia maonyesho hayo yaliyoanza Oktoba 30 hadi Novemba Mosi, 2026, wahudhuriaji waliotembela Banda la Ubalozi wa Tanzania walijibiwa maswali mbalimbali waliyouliza na kupata fursa za kupewa taarifa za utalii kuhusu safari za wanyamapori zinazotambulika duniani, mandhari ya kuvutia, fukwe safi na urithi wake tajiri wa kitamaduni na kuwahamasisha kutembelea vivutio mbalimbali vinavyopatikana.
Ubalozi huo ukiongozwa na Balozi Joseph Sokoine ulifanya kazi ya kuwahamasisha wahudhuriaji wa maonyesho hayo kutembelea na kuwahakikisha kwamba utalii wa Tanzania unafikika kwa urahisi.
Ushiriki wa maonyesho hayo umetoa fursa ya kuitangaza Tanzania zaidi Montréal ambako ni lango muhimu la kimkakati kuelekea soko la utalii la Québec na kujenga uhusiano na wasafiri wa Canada ambao kwa sasa wanashawishika kutembelea maeneo ya kitalii nje ya Amerika Kaskazini na Caribbean.
Wahudhuriaji wa banda la ubalozi huo wamepata fursa ya kuonja ladha ya Tanzania kupitia vitu vya utamaduni, mavazi ya jadi yaliyovaliwa na wawakilishi, masomo ya utangulizi ya Kiswahili yaliyohusisha maneno na misemo rahisi ya kila siku.
Pia wamejifunza kuhusu vyakula vya Tanzania na bidhaa muhimu zinazouzwa nje zikiwamo kahawa, chai na nyinginezo.
MWISHO





