Na Mwandishi Maalum, CMU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amekipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa utekelezaji mzuri wa mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Lindi.

Makamu wa Rais amesema ubora wa majengo yaliyojengwa unaonesha matumizi sahihi ya fedha za umma na thamani halisi ya fedha zilizowekezwa, huku ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi huo ukifikia asilimia 98.

Akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika eneo la Ngongo, Manispaa ya Lindi, Makamu wa Rais ameeeleza namna alivyovutiwa na ubora wa miundombinu iliyojengwa, akisema uwekezaji huo wa takribani Sh. bilioni 14 umeleta matokeo yanayoonekana. 

Aidha, amezitaka taasisi nyingine za umma kujifunza kutoka UDSM kuhusu namna bora ya kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.

“Nimevutiwa sana na namna Chuo Kikuu kilivyotekeleza mradi huu. Unapotazama majengo haya, unaona wazi kuwa fedha za takribani Sh bilioni 14 zimetumika vizuri. Hakika, hapa kuna thamani ya fedha iliyowekezwa. Nazihimiza taasisi nyingine kuja kujifunza kutoka UDSM namna ya kutekeleza miradi ya aina hii. Ninakipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa mafanikio haya,” amesema Makamu wa Rais.

Pongezi hizo zimeonesha kuridhishwa na usimamizi wa mradi, ufuatiliaji wa utekelezaji wake pamoja na ubora wa miundombinu iliyojengwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaotekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Aidha, Makamu wa Rais ameelekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoa kipaumbele kwa Kampasi ya Lindi katika awamu ya pili ya mradi HEET, hususan katika ujenzi wa nyumba za makazi kwa ajili ya wahadhiri na watumishi wa UDSM ili kuimarisha mazingira ya kazi na uwezo wa kampasi kutoa huduma zake kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameipongeza UDSM kwa hatua iliyofikiwa, akisisitiza umuhimu wa kukamilisha miundombinu hasa barabara za kuifikia kampasi hiyo pamoja na nyumba za watumishi.

Akizungumzia suala la barabara, Dkt. Kikwete alisisitiza kuwa kampasi inahitaji kuunganishwa vizuri na maeneo mengine ili kurahisisha upatikanaji wake, akieleza kuwa Serikali ina dhamira ya kushughulikia mahitaji yaliyosalia.

“Ujenzi wa kampasi hii ni mafanikio makubwa, lakini tunapaswa kuhakikisha kuwa miundombinu yote inayoiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi inakamilishwa. Barabara ni muhimu sana, na Serikali imejizatiti kushughulikia changamoto hii. Vilevile, tunapaswa kuangalia suala la nyumba za watumishi wetu ili wanaofanya kazi hapa wawe na mazingira mazuri ya kuishi na kutekeleza majukumu yao,” amesema Dkt. Kikwete.

Msisitizo huo unaonesha umuhimu wa kuendeleza kampasi hiyo kama jumuiya kamili ya kitaaluma, yenye miundombinu na huduma zinazowezesha ufundishaji, ujifunzaji, utafiti pamoja na ustawi wa watumishi na wanafunzi.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais alipokelewa na Dkt. Kikwete, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Prof. Rose Upor, pamoja na Naibu Mratibu wa HEET wa chuo hicho, Prof. Liberato Venant Haule.

Ujenzi wafikia asilimia 98

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi, Prof. Haule alisema ujenzi wa awamu ya kwanza umefikia asilimia 98, huku mkandarasi akitarajiwa kukabidhi majengo kabla ya Novemba 30, 2026, kufuatia kuongezwa kwa muda wa utekelezaji ili kukamilisha kazi zilizobaki.

Alisema kukamilika kwa kampasi hiyo kutakuwa na manufaa makubwa kwa chuo kikuu na jamii inayozunguka eneo hilo, hususan kwa kuongeza fursa za elimu ya juu, utafiti na shughuli za maendeleo ya kiuchumi.

“Ujenzi wa kampasi hii utaleta manufaa makubwa si tu kwa Chuo Kikuu, bali pia kwa jamii inayozunguka eneo hili,” alisema Prof. Haule.

Alifafanua kuwa mradi unahusisha ujenzi wa majengo sita katika eneo la Ngongo, Manispaa ya Lindi, pamoja na majengo mengine matatu katika Kituo cha Utafiti cha chuo hicho kilichopo Wilaya ya Ruangwa. Mradi huo unagharimu jumla ya Sh 14,795,722,687.72.

Kazi za ujenzi zinatekelezwa na kampuni ya M/s Shandong Hi-Speed Dejian Group Ltd, huku kampuni ya Geometry Consultants Limited ikisimamia na kushauri kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Katika eneo la Ngongo, miundombinu iliyojengwa inajumuisha jengo la utawala na taaluma lenye ofisi za watumishi na vyumba vitano vya mihadhara vinavyoweza kuchukua wanafunzi 390 kwa pamoja; maktaba; karakana yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 30; maabara tatu zenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 125; pamoja na mabweni mawili yenye nafasi za malazi kwa wanafunzi 200.

Nayo miundombinu ya Kituo cha Utafiti cha Ruangwa inajumuisha jengo la bweni, darasa na ukumbi wa chakula, vyenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 50.

Majengo hayo yanatarajiwa kutoa mazingira ya kisasa ya kujifunzia na kufanya utafiti, na hivyo kukiwezesha chuo kupanua programu zake za kitaaluma huku kikiimarisha mafunzo kwa vitendo na tafiti katika sekta za kilimo, ufugaji na maeneo mengine yanayohusiana na sekta hizo.

Miundombinu kuimarishwa

Pamoja na kazi kuu za ujenzi kufikia hatua za mwisho, chuo kinaendelea kushughulikia miundombinu mingine muhimu ili kuhakikisha kampasi inaanza kufanya kazi katika mazingira yanayokidhi mahitaji ya wanafunzi na watumishi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Prof. Haule, kampasi tayari imeunganishwa na huduma za maji na umeme. Wakati huohuo, ujenzi wa sehemu ya barabara yenye urefu wa mita 400 unaendelea chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA). Barabara hiyo ina urefu wa takribani mita 2,200.

Barabara hiyo ni muhimu katika kurahisisha usafiri wa kwenda na kutoka kampasini, kuwawezesha wanafunzi na watumishi kufika kwenye maeneo ya taaluma na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za chuo.

Vilevile, ujenzi wa nyumba za watumishi ni sehemu muhimu ya kuimarisha jumuiya endelevu ya kitaaluma, hasa wakati kampasi hiyo ikijiandaa kupokea wanafunzi wake wa kwanza na kuajiri watumishi watakaosimamia shughuli za kitaaluma na kiutawala.

Maandalizi ya majengo kwa ajili ya matumizi mengine nayo yanaendelea. Samani mbalimbali, zikiwemo vitanda, viti, kabati na meza, tayari zimewekwa. Vifaa vya maabara za Sayansi ya Mazao vilifika Dar es Salaam Novemba 9, 2026, na vilikuwa vikisubiri kukamilika kwa taratibu za forodha bandarini kabla ya kusafirishwa kwenda Lindi. Vifaa vya Uhandisi wa Kilimo vinatarajiwa kufika Dar es Salaam Novemba 28, 2026.

Kampasi kuongeza fursa za elimu ya juu Kusini mwa Tanzania

Zaidi ya uwekezaji wa miundombinu, Kampasi ya Lindi inatarajiwa kupanua kwa kiasi kikubwa fursa za elimu ya juu katika fani maalumu, huku ikichangia kukidhi mahitaji ya wataalamu katika sekta za kilimo, mifugo, teknolojia ya chakula na maeneo mengine yanayohusiana na sekta hizo.

Kampasi hii tayari imetambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), na programu nne za masomo zimeidhinishwa kuanza kutolewa. Programu hizo ni Shahada ya Sayansi ya Teknolojia ya Sayansi ya Mazao; Shahada ya Sayansi ya Teknolojia ya Nyuki; Stashahada ya Afya na Uzalishaji wa Mifugo; pamoja na Stashahada ya Teknolojia na Usimamizi wa Uzalishaji wa Mazao.

Shughuli za kitaaluma zitatekelezwa kupitia idara tano ambazo ni Sayansi ya Mazao na Teknolojia ya Ufugaji Nyuki; Uhandisi na Teknolojia ya Kilimo; Sayansi na Teknolojia ya Chakula; Uchumi wa Maliasili, Kilimo na Biashara; pamoja na Tiba ya Mifugo na Sayansi ya Wanyama.

Katika hatua ya awali, chuo kinatarajia kudahili wanafunzi 360 kuanzia Machi 2027, ambapo udahili wa kwanza utajikita katika programu mbili za shahada ya kwanza, ambazo ni Teknolojia ya Sayansi ya Mazao na Teknolojia ya Nyuki.

Katika mwaka wa masomo utakaofuata, chuo kinapanga kuanzisha programu nyingine mbili, ambazo ni Shahada ya Sayansi ya Teknolojia ya Sayansi ya Wanyama kwa Vitendo na Stashahada ya Teknolojia za Kuongeza Thamani ya Mazao ya Nyuki. Programu hizo zitaongeza nafasi nyingine 120 za udahili.

Mpango wa muda mrefu wa UDSM ni kupanua kampasi hiyo ili iweze kuhudumia wanafunzi 1,320 ifikapo mwaka wa masomo 2029/2030.

Programu hizo zimeandaliwa kimkakati ili kuimarisha mchango wa elimu ya juu katika mageuzi ya sekta ya kilimo kwa kuwaandaa wahitimu wenye maarifa ya kisayansi, ujuzi wa vitendo na uwezo wa kutumia teknolojia kuboresha uzalishaji, uchakataji na uongezaji thamani wa mazao.

Aidha, kampasi hiyo itatoa fursa za utafiti, ubunifu na huduma za kitaalamu za ushauri kwa wakulima, wafugaji, wajasiriamali na wadau wengine. Kupitia ushirikiano na taasisi za utafiti wa kilimo na mifugo, UDSM inalenga kuimarisha matumizi ya maarifa ya kisayansi katika kutatua changamoto za uzalishaji na kuongeza tija katika sekta hizo.

Kwa mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, kuanzishwa kwa kampasi hiyo ni hatua muhimu katika kusogeza karibu fursa za elimu ya juu kwa vijana, huku ikiimarisha uhusiano kati ya vyuo vikuu na sekta zinazozalisha mali na kuchochea uchumi wa maeneo hayo.

Mradi wanufaisha jamii kwa ajira na biashara

Manufaa ya kiuchumi ya mradi huo tayari yameanza kuonekana kwa jamii zinazozunguka eneo la ujenzi kupitia ajira na fursa za kibiashara zilizotokana na utekelezaji wake.

Taarifa ya mradi inaonesha kuwa jumla ya Watanzania 1,114 wamepata ajira tangu kuanza kwa ujenzi, wakiwemo wanawake 87. Aidha, wafanyabiashara na wananchi wa maeneo hayo wamenufaika kwa kupata fursa za kusambaza vifaa vya ujenzi na kutoa huduma mbalimbali, zikiwemo za chakula kwa wafanyakazi wa mradi.

Kampasi hii itakapoanza kufanya kazi kikamilifu, inatarajiwa kuchochea zaidi shughuli za kiuchumi kutokana na mahitaji ya malazi, usafiri, chakula, huduma za kifedha na bidhaa nyingine zitakazohitajika na wanafunzi, watumishi wa chuo na wageni.

Pia, kampasi hiyo itachangia kuandaa wataalamu wenye ujuzi kwa ajili ya sekta ya kilimo na viwanda vinavyohusiana nayo, kuimarisha ushirikiano katika tafiti na kutoa utaalamu wa kitaalamu utakaosaidia shughuli za kilimo na biashara katika mikoa ya kusini na maeneo mengine nchini.

Kampasi ya Lindi ni miongoni mwa uwekezaji wa kimkakati wa UDSM unaotekelezwa kupitia Mpango wa HEET kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania kupitia mkopo wa Benki ya Dunia. Mpango huo unalenga kuboresha na kuleta mageuzi katika taasisi za elimu ya juu ili ziweze kuchangia kwa ufanisi zaidi ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.

Kwa ujumla, Kampasi ya Lindi si upanuzi wa huduma za chuo kikuu kijiografia pekee, bali ni uwekezaji katika watu, maarifa, ubunifu wa kilimo na maendeleo ya uchumi wa kikanda. Kupitia kampasi hiyo, fursa za elimu ya juu zinasogezwa karibu zaidi na wananchi, huku UDSM ikiimarisha mchango wake katika mageuzi ya sekta ya kilimo na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya Tanzania.