Sumbawanga, Rukwa

Wananchi wa kijiji cha Kiyandaigonda, kata ya Kaoze Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa wamejawa na furaha kuelekea kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kiyandaigonda – Chombe yenye urefu wa kilomita 8.3.

Kijiji cha Kiyandaigonda ambacho ni maarufu kwa kilimo cha mpunga, mahindi, alizeti, mihogo na viazi miundombinu yake ya barabara imeharibiwa vibaya na mvua kutoka uwanda wa juu wa milima jirani na kijiji hicho ambayo imeharibu barabara na madaraja yote hivyo kusababisha changomoto ya mawasiliano ya barabara katika kijiji hicho.

Msimamizi wa mradi huo, Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Sumbawanga Mhandisi Christopher Shija amesema, ujenzi wa barabara hiyo unaotekelezwa na TARURA kupitia mradi wa CERC umeletwa kwa malengo mahsusi kwa ajili ya kuondoa adha ambayo wananchi wa kijiji cha Kiyandaigonda ambao kwa sasa wana furaha kubwa kutokana na maendeleo mazuri ya mradi huo ambao umefikia asilimia 87 ya utekelezaji wake.

“Kulikuwa na changamoto ya upitishaji mazao na hata uhaba na gharama ya juu kwa bidhaa muhimu hasa kwa wananchi wa Kiyandaigonde, Kaoze na Chombe, kwa hatua hii ya utekelezaji iliyofikiwa baadhi ya bidhaa zimeanza kupungua bei na mazao kama mchele bei zimeanza kupungua kutokana na magari kufika mashambani kwa urahisi” amesema Mhandisi Shija.

Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa madaraja na vivuko 18 ambapo madaraja makubwa matano na madogo ni 13 sambamba na upandishaji wa tuta la barabara lenye urefu wa km 8.3.

Ameongeza kuwa mpaka sasa jumla ya madaraja na vivuko 14 vimekamilika, vimebaki vivuko vitatu, unyanyuaji wa tuta la barabara km 8 nao umekamilika na hatua inayoendelea sasa hivi ni kuvisambaza ili kuweka changarawe kilomita zote 8.3

Kwa upande wake, Bw. Chrisant Kiliyaka Afisa Mtendaji wa kijiji cha Kiyandaigonda amesema kabla ya mradi huo walikuwa na changamoto nyingi ambazo zimewadhoofisha kiuchumi.

“Kukosa daraja na barabara ni vitu ambavyo vinaleta umaskini kwahiyo baada ya mradi huu wananchi wamefarijika sana, ndio mana wanapambana kuja kutoa maombi ya kimila ili kufanikisha kukamilika kwa daraja na barabara ili iweze kutuletea maendeleo katika kijiji chetu” amesema Bw. Kiliyaka.

Ameongeza kuwa kiuchumi barabara hiyo ni mkombozi kwao kwani itakapokamilika itawawezesha kuuza mazao yao kwa urahisi na bei itaongezeka kwa sababu magari makubwa yataweza kufika katika kijiji chao na kusafirisha mazao.