Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha
Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameeleza umuhimu wa kuimarisha Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) ili iweze kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya, kulinda haki, kuimarisha utawala wa sheria na kuweka mazingira rafiki kwa biashara na uwekezaji, huku wakisisitiza kuwa maamuzi yake yanapaswa kutekelezwa na nchi wanachama.
Wito huo umetolewa leo wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama hiyo yaliyofanyika Arusha, ambapo viongozi mbalimbali wameeleza kuwa ushirikiano wa kikanda hauwezi kufanikiwa kwa kutegemea makubaliano ya kisiasa na kiuchumi pekee, bali unahitaji taasisi imara, huru na zenye uwezo wa kuhakikisha sheria na masharti ya Jumuiya yanaheshimiwa.
Akifungua maadhimisho hayo, Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC, Rebecca Kadaga, amesema nchi za Afrika zinapaswa kuondokana na mifumo ya kiuchumi iliyozifanya kuwa na masoko madogo na badala yake kuimarisha ushirikiano utakaowezesha bidhaa na huduma kusambazwa katika ukanda mzima.
“Nchi moja haiwezi kutumia kikamilifu bidhaa zote zinazozalishwa ndani ya mipaka yake, kwa mfano mkulima wa Masaka nchini Uganda anayezalisha maziwa, viwanda vya Kenya vinavyozalisha saruji na viwanda vya Dar es Salaam vinavyozalisha nguo kwani maendeleo ya kweli yanahitaji soko kubwa la pamoja litakalounganisha uzalishaji na mahitaji ya wananchi wa nchi wanachama”
Ametolea mfano mataifa makubwa kama Marekani, China na India kwamba yameweza kuimarisha uchumi wake kutokana na kuwa na masoko makubwa, hivyo Afrika Mashariki inapaswa kutumia fursa ya soko lake la pamoja kukuza biashara, viwanda, uwekezaji na ajira badala ya kuendelea kuweka vikwazo vinavyokwamisha biashara kuvuka mipaka.
Akieleza umuhimu wa Mahakama hiyo Kadaga amesema ilianzishwa kuwa mlezi na msimamizi wa Mkataba wa Jumuiya, kuhakikisha nchi wanachama zinafuata makubaliano yaliyowekwa, akionya kuwa hakuna kiongozi au afisa anayepaswa kuzuia bidhaa kuvuka mipaka bila sababu za msingi kwa kuwa hatua hiyo inakiuka misingi ya Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja.
Kadaga amesisitiza kuwa haki inapaswa kwenda sambamba na maendeleo ya kiuchumi na kijamii, akionya dhidi ya matumizi ya mifumo ya kisheria bila kuzingatia mazingira halisi ya Afrik hasa pale maamuzi ya kimahakama yanapoweza kuchelewesha miradi ya maendeleo kwa muda mrefu kutokana na changamoto ndogo za kiutaratibu.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, Jaji Nestor Kayobera, amesema kuanzishwa kwa Mahakama hiyo kulilenga kuweka taasisi huru ya kimahakama yenye jukumu la kutafsiri Mkataba wa Jumuiya, kusimamia utawala wa sheria na uwajibikaji akisisitiza kuwa ushirikiano wa kikanda hauwezi kudumu kwa kutegemea dhamira ya kisiasa na ushirikiano wa kiuchumi pekee bila kuwepo mfumo madhubuti wa kusimamia sheria.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi, amesema hadi kufikia Oktoba 26 mwaka huu, Mahakama hiyo ilikuwa imesajili jumla ya mashauri zaidi ya elfu moja tangu kuanzishwa kwake, jambo linaloonesha kuongezeka kwa imani ya wananchi na taasisi katika Mahakama hiyo kama chombo cha kutatua migogoro inayotokana na Mkataba wa Jumuiya.
Balozi Mbundi amesema katika kipindi hicho, Jumuiya imepiga hatua kwa kuanzisha Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja, huku ikiendelea na maandalizi ya Umoja wa Fedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
“Ni muhimu kuimarisha matumizi ya usuluhishi wa migogoro kupitia majadiliano, maridhiano na mifumo ya kisheria ili kupunguza gharama, kuongeza imani ya wawekezaji na kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa haki na ufanisi”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ofisi ya Kikanda ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, Mamadou Balde, amesema wakimbizi hawapaswi kutazamwa kwa mtazamo wa misaada ya kibinadamu na changamoto za kiusalama pekee, bali wanapaswa kutambuliwa kama watu wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo wanayohifadhiwa.
Amesema ni muhimu kuweka mifumo itakayowawezesha kushiriki katika shughuli za uzalishaji, kujenga maisha na kutumia uwezo wao kuchangia maendeleo ya jamii.
“Takwimu zinaonesha kuwa takribani watu milioni 4.6 wamehama makazi yao ndani ya mataifa ya Afrika, hali inayohitaji hatua zinazozingatia utu, haki na ushirikiano wa kikanda na katika miaka 25 ijayo na matarajio ni kuona Mahakama imara zaidi na Afrika yenye mshikamano, inayolinda haki za kila mtu bila kujali hali yake ya uraia au mazingira”




