NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Posta Tanzania limeanza kuweka msisitizo mpya katika uwajibikaji wa viongozi wake, likieleza kuwa utendaji wa mameneja utapimwa kwa mafanikio wanayoyapata katika kukuza biashara na kuboresha huduma.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa mameneja wa Mikoa Posta Tanzania, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbodo amesema viongozi watakaoshindwa kutimiza majukumu yao watawajibishwa baada ya tathmini ya utendaji, akibainisha kuwa hakuna atakayekuwa nje ya wigo wa mchakato huo, wakiwemo viongozi wa makao makuu.
Alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa mameneja wa mikoa kuhusu utendaji unaozingatia matokeo kwa lengo la kuongeza uzalishaji, yanayofanyika katika makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam, Novemba 12 hadi 13, 2026.
Alisema tathmini hizo zitakuwa za haki na kuzingatia matokeo ya kila eneo, huku watendaji wanaofanya vizuri wakitambuliwa na maeneo yenye changamoto yakifanyiwa uchambuzi ili kubaini hatua zinazofaa za kuboresha utendaji.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika baadhi ya mikoa, alitolea mfano Mkoa wa Morogoro ambao umefanikiwa kupata fursa kubwa ya biashara ya usafirishaji wa vifurushi, hali iliyosababisha changamoto ya upungufu wa magari ya kuhudumia mahitaji yaliyopo.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya baadhi ya mikoa yanapaswa kuwa chachu kwa mingine kujifunza na kubuni mikakati mipya ya kibiashara, badala ya viongozi kujifungia katika mitazamo inayozuia ubunifu na matumizi ya fursa zilizopo.
Katika hatua nyingine, alisema Shirika la Posta Tanzania limepiga hatua katika ushindani wa kimataifa baada ya kushika nafasi ya 66 duniani na ya nne barani Afrika katika tathmini ya Umoja wa Posta Duniani, likitanguliwa na Misri, Morocco na Mauritius.
Hata hivyo, alisema shirika hilo halitaridhika na mafanikio hayo, bali linaendelea kuweka mikakati ya kuimarisha ushindani wake ili kuwa kinara wa huduma za posta barani Afrika.
Alieleza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Posta Duniani ameonesha matarajio ya Tanzania kuwa kinara wa sekta hiyo kutokana na kasi ya mageuzi yanayoendelea nchini.
Postamasta Mkuu aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia maarifa watakayoyapata kuboresha usimamizi wa biashara, matumizi ya rasilimali, uwajibikaji wa watumishi na utoaji wa huduma bora kwa wateja.
Alisisitiza kuwa mageuzi hayo yanahitaji ushiriki wa kila mtumishi, akieleza kuwa Shirika la Posta Tanzania linamilikiwa na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha linaendelea kukua na kutoa huduma zenye tija.


