Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema amani na umoja ni msingi wa maendeleo endelevu na ustawi wa nchi, akieleza kuwa biashara, uwekezaji, utalii na shughuli nyingine za kiuchumi zinahitaji mazingira salama na tulivu ili kustawi.

Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo tarehe 11 Novemba 2026, katika Hafla ya Usiku wa QURAAN iliyoandaliwa na Jumuiya ya Bohra Tanzania katika Msikiti wa Hakimi, Upanga, Dar es Salaam.

Amesema Tanzania imeendelea kujenga taifa lenye umoja miongoni mwa wananchi wenye tamaduni na mila mbalimbali, akieleza kuwa utofauti huo ni utajiri na nguvu ya Taifa. Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza maadili ya kuvumiliana, kuheshimiana na kuishi kwa maelewano katika familia, jamii, shule na taasisi za dini.

Dkt. Mwinyi amewapongeza viongozi wa dini kwa mchango wao katika malezi ya jamii, na kuwataka kuendelea kutumia nyumba za ibada kuwa vituo vya mwongozo wa kiroho, maadili na maridhiano, pamoja na kuhimiza utatuzi wa tofauti kwa njia ya mazungumzo.

Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, bandari na umeme, pamoja na kuimarisha huduma za afya na elimu, sambamba na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, akibainisha kuwa mafanikio ya juhudi hizo yanategemea kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu nchini.

Aidha, amewahimiza vijana kuzingatia elimu, kujenga ujuzi, kushiriki katika ujasiriamali na kutumia fursa za kiuchumi, huku wakidumisha nidhamu, uadilifu na uzalendo ili kuwa sehemu ya maendeleo ya Taifa.

Hafla hiyo imepambwa kwa qaswida mbalimbali za kumsifu Mtume Muhammad (S.A.W), sambamba na usomaji wa QURAAN Tukufu uliofanywa na washiriki mbalimbali, wakiwemo vijana mahafidhi na wanafunzi wa taasisi za Kiislamu.

Rais Dkt. Mwinyi pia ameshiriki chakula cha pamoja cha Jumuiya (Community Kitchen) pamoja na viongozi, waumini na wageni waliohudhuria hafla hiyo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwemo Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Mhe. Juma Malik Akil, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar; Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Afya Zanzibar; pamoja na Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally, Mufti Mkuu wa Tanzania.

Wengine ni Sheikh Zoebbhai Galiakotwalla, mwakilishi wa Jumuiya ya Bohra Dar es Salaam; Qussay Bhai Saheb Jamaludin, mwakilishi wa Sheikh Syedna Mufaddal Saifuddin, Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Dawoodi Bohra Duniani, pamoja na wageni waalikwa kutoka sehemu mbalimbali duniani.