📌Ni baada ya kumshinda Bondia Kurta Pabular kutoka Ufilipino

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetumia mashindano ya ngumi yaliyofanyika The Super Dome Masaki kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme na kuhamasisha michezo nchini.

TANESCO imetumia nafasi hiyo kumzawadia bondia Kalolo Amiri kutoka Tanzania kiasi cha Shilingi Milioni Mbili pamoja na jiko la kisasa la umeme (Smart Pika), kufuatia ushindi dhidi ya mpinzani wake Kurta Pabular kutoka Ufilipino.

Akikabidhi zawadi hizo Novemba 13, 2026, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Wadau, Augustino Kasale, amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Shirika za kuendelea kuunga mkono sekta ya michezo kwa kutambua mchango wa wanamichezo wanaolitangaza Taifa kupitia mashindano ya kimataifa.

Amesema TANESCO imemzawadia bondia huyo fedha taslimu pamoja na jiko la umeme ambalo linatumia umeme kidogo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme.

“TANESCO inaendelea kuunga mkono michezo nchini. Tumetoa Zawadi hizi kwa sababu tunatambua mchango wa wanamichezo wanaolitangaza Taifa letu. Pia tunaendelea kutumia majukwaa mbalimbali kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kutumia nishati ya umeme kupikia lengo ni kuongeza idadi ya wananchi wanaotumia nishati safi, “ ameeleza Bw. Kasale

Kwa upande wake, bondia Kalolo Amiri ameishukuru TANESCO kwa mchango wake katika michezo hasa mchezo wa ngumi ambapo amesema hatua hiyo inaongeza ari ya kuendelea kufanya vizuri katika mashindano yajayo.

“Namshukuru sana Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kwa kuona umuhimu wa kutambua mchango wetu katika michezo. Hatua hii imetupa nguvu zaidi ya kujituma na kujiandaa vizuri kwa mapambano yajayo, hususan yale yanayohusisha kuiwakilisha nchi yetu,” amesema Kalolo.

Katika pambano hilo, bondia Kalolo Amiri aliibuka mshindi kwa pointi dhidi ya Kurta Pabular kutoka Ufilipino katika pambano la raundi nane (Round 8), lililokuwa sehemu ya mashindano yaliyohusisha mapambano ya mabondia mbalimbali.

Mgeni rasmi katika mashindano hayo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo.