Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mkuranga
WANANCHI wa Kata ya Kisiju wilayani Mkuranga mkoani Pwani wameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa Bandari ya Kisiju, wakieleza kuwa kuchelewa kwa mradi huo kwa muda mrefu kumeendelea kuwa kero na kuwaacha katika sintofahamu kuhusu hatma yake.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara wakati wa ziara ya siku moja ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, wananchi Kajumlo Mhidini na Afishi Kimo walisema wanahitaji mradi huo utekelezwe ili kuondoa changamoto zinazowakabili na kuchochea maendeleo ya eneo hilo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kisiju, Ally Dau, alisema bandari hiyo ina umuhimu mkubwa katika kukuza uchumi wa eneo hilo, huku akisisitiza pia umuhimu wa kupatikana kwa boti ya uokozi baharini kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na dharura zinazotokea majini.
Akijibu kilio hicho, Nyongo amewahakikishia wananchi kuwa atalibeba na kulisimamia suala hilo chini ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitoa tamko kuwa ujenzi wa bandari hiyo unatarajiwa kuanza mwaka 2027.
Alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa gati litakalosogea zaidi ya kilomita moja ndani ya bahari kufikia eneo lenye kina kirefu cha maji, ili meli ziweze kupakia na kupakua mizigo muda wote bila kuathiriwa na maji kupwa na kujaa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Rajabu Msiku, alisema utafiti wa mradi huo katika eneo la Dindini, Kisiju, umekamilika na kwa sasa wanaendelea na taratibu za manunuzi ili kumpata mkandarasi.
Katika ziara hiyo pia Nyongo ameielekeza Halmashauri ya Mkuranga kuhakikisha inasimamia na kuharakisha ujenzi wa Shule ya Sekondari Mbezi Gongoni ili ikamilike kwa wakati na kuanza kupokea wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2027.
Aidha, aliitaka Halmashauri hiyo kukamilisha taratibu za usajili wa shule hiyo mapema ili kuwezesha kuanza kwa shughuli za utoaji wa elimu mara baada ya kukamilika kwa miundombinu inayohitajika.
Alisisitiza umuhimu wa Halmashauri kutenga fedha kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, yatakayowasaidia wanafunzi wanaoishi mbali na shule hiyo kupata mazingira salama ya kujifunzia na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuathiri maendeleo yao ya kitaaluma.
Awali, akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mtendaji wa Kijiji cha Msufini Kidete, Beatrice Anthony Deref, alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule hiyo ulianza Juni 2024 na kukamilika Juni 2026 kwa gharama ya Sh milioni 196.2 zilizotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Alisema mradi huo unalenga kuongeza nafasi za wanafunzi kujiunga na elimu ya sekondari mwaka 2027 na 2028, kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kupunguza adha ya wanafunzi wa Kata ya Mbezi ambao wamekuwa wakitembea zaidi ya kilomita tano kufuata elimu katika Shule za Sekondari Shungubweni na Kitumbo.





