Na Mwandishi Wetu, Kagera

Afisa Afya wa Mkoa wa Kagera, Ndugu Yassin Mwinori, amewaagiza wamiliki wa shule za bweni mkoani humo kuhakikisha wanafanya usafi wa kina na kupulizia dawa za kuangamiza wadudu waharibifu wakiwemo kunguni na viroboto kabla ya Desemba 20 mwaka huu.

Mwinori ametoa agizo hilo leo Novemba 13, 2026, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuzuia mazalia ya wadudu na kulinda afya za wanafunzi. Amesisitiza kuwa shule zinapaswa pia kupaka rangi upya mabweni na vitanda pamoja na kuhakikisha usafi unafanyika mara kwa mara.

Aidha, amewaagiza maafisa afya wa halmashauri kukagua maghala ya chakula ili kuhakikisha vyakula vinahifadhiwa katika mazingira salama na kuondoa vile vilivyoharibiwa na wadudu. Pia, shule zinapaswa kusafisha visima vya maji na mifereji ya maji ya mvua pamoja na kutumia klorini kuhakikisha maji yanayotumiwa na wanafunzi ni salama.

Amesema ifikapo Desemba 20, maafisa afya wa halmashauri zote nane wanapaswa kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa agizo hilo, huku ukaguzi wa pamoja kati ya Idara za Afya na Elimu ukifanyika kuanzia Desemba 21 hadi Januari 15. Shule zitakazobainika kutotekeleza maelekezo hayo hazitaruhusiwa kupokea wanafunzi hadi zitakapoweka mazingira katika hali inayokidhi viwango vya usalama, huku wamiliki wakitakiwa kuwasilisha vyeti vya uthibitisho wa zoezi la fumigation kutoka kampuni zilizoidhinishwa kisheria.