Na Mwandishi Wetu, Rukwa

WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekamilisha mradi wa ujenzi wa daraja la mawe la Natene linalounganisha Kata ya Namanyele na Isunta, Halmashauri ya Nkasi, mkoani Rukwa.

Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 44 ambalo limekamilika kwa asilimia 100 umetokana na changamoto ya uvukaji katika mto Natene ambao ulizitenganisha kata hizo kwa muda mrefu na kuwafanya wananchi wa pande zote mbili kupata usumbufu mkubwa kuvuka hasa wakati wa masika.

Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Nkasi Mhandisi Madirisha Lumala amesema hapo awali hapakuwa na daraja katika mto huo na kwamba mto huo ulikuwa umewatenganisha wakazi hao.

“Ukiangalia hizi kata zinaingiliana. Kila upande kuna shule za sekondari na msingi ambapo wanafunzi wanatoka kata ya Namanyele kwenda kusoma shule ya Msingi Isunta na kuna ambao wanatoka Isunta kwenda kusoma shule ya sekondari ya Mkangale ambayo ipo kata ya Namanyele.”

“Lakini kipindi cha masika mawasiliano hukatika baada ya mto Natene kujaa maji. Kutokana na adha hiyo serikali ikaona kuna ulazima wa kujenga daraja, ingawa kulikuwa na daraja la muda lakini halikuwa salama kwani kuna taarifa za wananchi kupoteza maisha wakiwa wanajaribu kuvuka kupitia daraja hilo hivyo Serikali ikaleta fedha na kujenga daraja hili.” amefafanua Mhandisi Madirisha.

Aliongeza daraja hilo lenye urefu wa mita 44 limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 192 kwa kutumia teknolojia mpya ya ujenzi wa mawe.

Aidha, Mhandisi Madirisha alisema matumizi ya teknolojia hiyo yameweza kuokoa fedha nyingi kama wangetumia teknolojia ya zege na nondo ambapo makadirio ya gharama yanaonesha kufika shilingi bilioni 3.5 hadi bilioni 4.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Namanyele Bw. Crispin Wikula aliishukuru Serikali chini ya uongozi wa Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha ujenzi wa daraja hilo kwani limeondoa kero kwa wananchi kuzifikia huduma za kijamii kama vile shule, makanisa, misikiti na hospitali kwa urahisi hasa kipindi cha masika.

Naye, Bi. Christina Kalungizi mkazi wa Mabatini mjini Namanyele amemshukuru Mama Samia kwa kuwajengea daraja kwani sasa hivi wanavuka kwa furaha na amani hata usiku wakipata dharura wanaita boda boda na kuwabeba bila shida na kwa gharama nafuu.