Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mhandisi Innocent Luoga, amesisitiza umuhimu wa kuwa na taarifa sahihi za kijiolojia zitakazosaidia kutoa uhakika kuhusu maeneo yenye uwezekano wa kuwapo kwa mafuta na gesi asilia, pamoja na kuongeza mvuto wa sekta hiyo kwa wawekezaji.

Amesema hayo leo Novemba 16, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi katika Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), kilichofunguliwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa katika kuboresha upatikanaji wa taarifa hizo, Mhandisi Luoga amesema PURA imeweka kipaumbele katika kuongeza upatikanaji wa taarifa za kijiofizikia katika maeneo ya nchi kavu na bahari yenye kina kifupi ili kuongeza uelewa kuhusu rasilimali zilizopo na kuvutia uwekezaji zaidi.

Amebainisha kuwa PURA imefanya mazungumzo na kampuni ya Geopartners kwa ajili ya kushirikiana nayo katika masuala yatakayowezesha kupatikana kwa taarifa hizo muhimu.

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Wizara yaliyotolewa Februari 2026, ambapo PURA ilielekezwa kuandaa mkakati wa kufanya tafiti za awali za utafutaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na kubaini maeneo mapya yanayoweza kufanyiwa shughuli za utafutaji.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Luoga ameipongeza PURA kwa juhudi inazoendelea kuchukua katika kuimarisha usimamizi wa sekta ya mafuta na gesi asilia nchini pamoja na kutekeleza maelekezo ya Wizara.

Sambamba na hilo, ameitaka PURA kuendelea kuimarisha uwajibikaji, ufuatiliaji wa maazimio ya Baraza, weledi wa utendaji, usalama mahali pa kazi, utunzaji wa mazingira na ushirikishwaji wa Watanzania katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli.