
Na John Mapepele, Mafia
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amemtaka Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Grace Magembe kuunda Kamati ya uchunguzi ili kuchunguza utolewaji wa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Mafia ili kuboresha huduma katika hospitali hiyo.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Novemba 16, 2026 baada ya kufanya ziara ya kikazi na kukagua maeneo mbalimbali ya Hospitali hiyo ambapo hakuridhishwa na utendaji kazi.

Ninamuelekeza Katibu Mkuu kuunda timu kuja kufanya uchunguzi na kubaini changamoto ili kuja na suluhisho la maboresho ya kudumu katika hospitali
Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuifanya hospitali hiyo kutoa huduma za afya kwa kiwango cha kisasa na kuachana na mazoea.

amefafanua sababu za kuifanya Hospitali hiyo kutoa huduma kwa kiwango cha kisasa kuwa ni pamoja na sehemu ya kisiwa hicho kuwa na Hifadhi ya Bahari ambayo huleta wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani.
“Sote tunajua eneo hili la mafia ni eneo la kimkakati katika nchi yetu lina Hifadhi ya Bahari ambayo inatembelewa na watalii wengi hivyo pindi wanapopata shida za kiafya lazima tuwe na hospitali inayoweza kutoa huduma ya uhakika tofauti na sasa”. Ameongeza Mhe. Mchengerwa

Aidha, ameitaja sababu nyingine kuwa kisiwa cha Mafia kipo pembeni mwa Tanzania bara na bado hakuna usafiri wa uhakika hivyo ni muhimu kuwa na huduma zilizoboreka.
Ametoa wiki mbili kwa uongozi wa hospitali hiyo kufunga mashine za kisasa za X-ray ambazo imepelekwa kwenye zahanati ya Chole.

“Naelekeza ile X-ray Mashine ya kisasa ambayo haijafungwa kwenye zahanati ya Chole sasa ije ifungwe hapa kwa kuwa hapa kuna uhitaji zaidi kuliko kule.” amesisitiza Mhe. Waziri Mchengerwa
Katika ziara hiyo ambayo aliambatana na Mkurugenzi wa Idara Kinga Dkt. Hamad Nyembea alipata fursa ya kuongea na wagonjwa waliofika kutibiwa.


