Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dodoma
Sekta ya fedha hapa nchini imeendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi na upanuzi wa fursa za biashara na uwekezaji kwa wananchi kupitia soko la mitaji, ambapo idadi ya wafanyabiashara na wawekezaji imeongezeka kwa asilimia 36.6 na kufikia 903,088 hadi mwishoni mwa Oktoba 2026, huku thamani ya mtaji wa soko ikifikia TZS trilioni 40 kwa mara ya kwanza katika historia yake.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha Kikundi Kazi cha Fedha cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), kilichofanyika jijini Dodoma jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi Kazi hicho, Dkt. Natu Mwamba, alisema ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa ufanisi na ubora wa huduma na bidhaa zinazotolewa katika soko la mitaji.
“Uwepo wa soko la mitaji unamwezesha mwananchi kupata fursa ya kushiriki katika umiliki wa uchumi na kukuza kipato chake kupitia ununuzi wa hisa na hatifungani, sambamba na kuimarisha sekta ya fedha na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,” alisema Dkt. Mwamba.
Alisema kuboreshwa kwa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwemo mfumo wa uwekezaji wa kidijitali wa soko la hisa (DSE) Hisa Kiganjani, kumerahisisha upatikanaji wa huduma za uwekezaji kwa Watanzania wengi zaidi na kuwawezesha kuwekeza saa 24 kwa siku.
“Mpaka sasa thamani ya mtaji wa soko imefikia Sh trilioni 40 kwa mara ya kwanza katika historia ya soko,” alisema Dkt. Mwamba.
Alifafanua kuwa miongoni mwa majukumu ya Kikundi Kazi hicho ni kuishauri Serikali na sekta binafsi kuhusu namna bora ya kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha katika uchumi, hususan katika sekta za kimkakati, pamoja na kutafuta njia za kupunguza viwango vya riba katika masoko ya fedha, hasa riba za mikopo kwa sekta binafsi.
Alisema Serikali inaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili yawe rafiki na wezeshi, sambamba na kupanua wigo wa walipa kodi kwa kuwafikia wafanyabiashara na wawekezaji wanaoendesha shughuli zao nje ya mfumo rasmi.
“Serikali inaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili yawe rafiki na wezeshi, sambamba na kuongeza idadi ya walipa kodi, wakiwemo wafanyabiashara ambao wanaendesha shughuli zao nje ya mfumo rasmi,” alisisitiza Dkt. Mwamba.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti Mwenza wa Kikundi Kazi hicho kutoka sekta binafsi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Bw. Geofrey Mchangila, alisema kikao hicho kilipitia taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita na kujadili mapendekezo mbalimbali ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Alisema moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele ni kuimarisha elimu ya fedha na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za soko la mitaji ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uwekezaji na kunufaika na ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Katika kikao hiki tumeangazia namna ya kuimarisha elimu ya fedha na uelewa kuhusu soko la mitaji, kwani kwa kufanya hivyo tutawawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uwekezaji na kunufaika na ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema Bw. Mchangila.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na kufanya uhamasishaji kwa wananchi, wakiwemo wafanyabiashara wadogo na wa kati, kuhusu soko la mitaji na fursa zilizopo ili kujenga uchumi shirikishi, kuongeza utajiri wa wananchi na kuhakikisha manufaa ya ukuaji wa uchumi yanafika hadi kwa mtu mmoja mmoja.
Naye Dkt. Godwill Wanga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), alisema kikao hicho kilijadili ajenda mbalimbali za kimkakati zinazolenga kuimarisha sekta ya fedha na mazingira ya uwekezaji nchini.
Alizitaja ajenda hizo kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa Kituo cha Kimataifa cha Fedha cha Dar es salaam nchini (DIFC), Uanzishwaji wa Shilingi ya Kidijitali ya Benki Kuu ya Tanzania (Central Bank Digital Currency-TZS), pendekezo la kuanzisha Soko la Kimataifa la Madini ndani ya DIFC, ikijumuisha biashara ya madini, huduma za kifedha, upatikanaji wa mitaji, miundombinu ya miamala na mahitaji ya kisheria ya kiudhibiti na Kiusalama.
Ajenda zingine ni utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini, uimarishaji wa mifumo ya upatikanaji na ukopeshaji wa fedha kwa riba nafuu kwa kampuni changa (Startups), Utekelezaji wa Dira 2050 katika Sekta ya Fedha na uboreshaji wa mifumo ya kidigitali na namba ya NIDA (Jamii Namba) ambayo itaunganishwa na mzunguko wa fedha (mapato na matumizi) nchini.
“Moja ya majukumu yetu kama TNBC ni kujenga uwezo wa sekta binafsi kwa kuweka mazingira wezeshi yanayopunguza gharama za biashara na uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi endelevu na jumuishi kwa watu wote kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa TNBC,” alisema Dkt. Wanga.
Kwa muktadha huo, TNBC itaendelea kufanya vikao vya kikundi Kazi cha Fedha kinachoongozwa na Wizara ya Fedha vitafanyika mara kwa mara kujadili changamoto na fursa zilizopo na kushauri Serikali na sekta binafsi ipasavyo, alisistiza Dkt. Wanga.





