Kamishna wa Elimu nchini Dkt. Lyabwene Mutahabwa leo tarehe 20 novemba, 2026 jijini Dar es Salaam amezindua rasmi Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Uongozi wa Shule nchini, hatua inayolenga kuboresha usimamizi wa elimu na kuongeza ubora wa matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji. 

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Dkt. Mutahabwa akimwakilisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Hussein Mohammed, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amesisitiza kuwa, uongozi bora wa shule ni nguzo muhimu katika kuboresha ubora wa elimu, kwani huweka mazingira wezeshi kwa walimu kufundisha kwa weledi na wanafunzi kujifunza kwa ufanisi. 

“Uzinduzi wa Kikosi Kazi hiki ni hatua muhimu katika kuimarisha uongozi wa shule, kuboresha matokeo ya ujifunzaji na kufanikisha matarajio ya Tanzania katika sekta ya elimu. Ni matarajio yetu kama Wizara kuwa, kitafanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa ili kufikia azma ya Serikali ya kuimarisha Uongozi bora wa Shule”. Amesema Dkt. Mutahabwa

Ameongeza kusema, maendeleo katika elimu yanaletwa na elimu bora, na elimu bora inahitaji walimu bora na mahiri, na walimu bora wanahitaji uongozi bora ili kufikia mafanikio ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni. 

Nae, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu – ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid akizungumza katika hafla hiyo amesema Kikosi Kazi hicho kitakuwa jukwaa la kimkakati la kuishauri Serikali kuhusu Sera na mikakati ya maendeleo ya uongozi wa shule. 

“Ni imani yetu kuwa kikosi kazi hiki kitasaidia kuendeleza viwango vya kitaaluma vya viongozi wa shule, kukuza tafiti na ubunifu, pamoja na kuimarisha mafunzo endelevu kwa wakuu wa shule na wasimamizi wa elimu”

Aidha, Dkt. Maulid ameongeza kuwa kupitia jukwaa hilo wamefanikiwa kuanzisha uhusiano na Vyuo Vikuu vinne kutoka nchini Zambia, Botswana, Namibia na Zimbabwe ambavyo vimefika nchini kwa ajili ya kujenga ushirikiano na Vyuo vikuu na Vyuo vya Kati vya nchini Tanzania ili kwa pamoja washirikiane kuleta mageuzi endelevu katika sekta ya elimu.

Amebainisha kuwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa baina ya Vyuo hivyo, utatoa fursa za kubadilishana uzoefu, kufanya tafiti za pamoja, kuanzisha programu za mafunzo na kujenga vituo vya umahiri katika eneo la uongozi wa elimu ili kujenga mfumo wa elimu unaozingatia ubora, ubunifu, uwajibikaji na ujifunzaji endelevu.

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu – ADEM inashirikiana na Taasisi ya African Centre for School Leadership – ACSL kutekeleza  mpango Mkakati wa kuimarisha uongozi na usimamizi wa shule nchini ambapo moja ya mpango wa kutekeleza hilo ni uundwaji rasmi Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Uongozi wa Shule nchini Tanzania kilichozinduliwa leo.

#UongoziWaShule #ElimuTanzania #UboraWaElimu #SchoolLeadership #EducationalLeadership #UshirikianoWaKikanda