Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amezipongeza kampuni za OffGridSun na Tango Energy kwa mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia usambazaji wa majiko banifu, uzalishaji wa ajira na uwekezaji nchini.
Pongezi hizo amezitoa leo Novemba 20, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Wakurugenzi wa kampuni hizo, Bi. Valentina Quaranta wa OffGridSun na Bw. Mussa Msofe wa Tango Energy Limited, kuhusu mipango yao ya kuendeleza ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kampuni hiyo, Mkurugenzi wa OffGridSun, Bi. Valentina Quaranta, amesema kampuni imejipanga kusambaza majiko banifu 300,000 ifikapo mwaka 2029, ambapo hadi sasa zaidi ya majiko 100,000 tayari yamesambazwa bure kwa wananchi katika mikoa ya Kigoma, Tanga, Dodoma, Morogoro na Arusha.
Amefafanua kuwa majiko hayo yamesambazwa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo majiko 10,000 Mkoa wa Kigoma, 18,500 katika Mkoa wa Tanga wilayani Handeni, 60,000 katika Wilaya za Chamwino na Kongwa mkoani Dodoma, 5,000 Ifakara mkoani Morogoro na 11,000 katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha.
Aidha, amesema mradi huo tayari umewafikia zaidi ya wananchi 500,000, huku kampuni ikilenga kuwafikia takribani wananchi milioni 1.5 ifikapo mwaka 2029.
Amesema kampuni hiyo pia, imechangia kukuza ajira kwa vijana zaidi ya 100 wanaopatiwa mafunzo mbalimbali ili kuwawezesha kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tango Energy Limited, Bw. Mussa Msofe, amesema kampuni hiyo imezalisha majiko banifu zaidi ya 97,331 ambayo yamesambazwa kwa wananchi katika mikoa ya Dodoma, Tanga, Kigoma, Katavi, Singida na Lindi, na kuwawezesha kupata teknolojia safi, salama kwa afya na rafiki kwa mazingira.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo imeingia makubaliano ya kimkakati na OffGridSun ya kuzalisha majiko banifu 300,000, huku ikiendelea kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania 175.
Vilevile, amesema kampuni hizo zimewekeza jumla ya shilingi bilioni 2.2 katika ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza majiko banifu kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, ambacho kinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa majiko hayo nchini na kuzinduliwa rasmi mwezi Februari 2027.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hizo, Waziri Homera amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini.
Aidha, amezitaka kampuni hizo kuendelea kuongeza kasi ya uzalishaji na usambazaji wa majiko banifu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kunufaika na teknolojia hiyo inayochangia kulinda afya, mazingira na kukuza maendeleo ya kiuchumi.






