Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
WATU watatu wamejeruhiwa katika ajali ya magari mawili kugongana iliyotokea eneo la Chamkweza, njia panda ya mnadani, Tarafa ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
Ajali hiyo imetokea Novemba 20, 2026, majira ya saa 7:50 asubuhi, ikihusisha basi la Sarotoga lililokuwa likitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam na gari aina ya Yutong lenye namba za usajili T.453DCX, lililokuwa likitokea Kigoma kuelekea Dar es Salaam.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Kennedy Mgani alieleza kuwa gari aina ya Yutong lilikuwa likiendeshwa na Ailly, mwenye umri wa miaka 47, mkazi wa Kigoma, huku basi la Sarotoga likiwa limeendeshwa na John Kisingi, mwenye umri wa miaka 34, aliyekuwa akitokea Dar es Salaam kuelekea Arusha.
Mgani alifafanua, katika ajali hiyo, watu watatu waliokuwa kwenye basi la Sarotoga wamejeruhiwa, akiwemo Mrina Mtambuka, mwenye umri wa miaka 33, mkazi wa Kibaha, Mkoa wa Pwani; Haruna Yusuf, mwenye umri wa miaka 47, mkazi wa Kigoma; pamoja na Hamada Shabani, mwenye umri wa miaka 35, mkazi wa Kigoma ambaye ni kondakta wa basi la Sarotoga.
Majeruhi wote wamepelekwa katika Kituo cha Afya Chalinze kwa matibabu zaidi.
Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi la Kampuni ya Sarotoga kuyapita magari mengine bila kuwa na tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara, ambaye alikimbia baada ya kusababisha ajali.
Mgani alisisitiza kwamba, dereva huyo anapaswa kujisalimisha katika kituo cha polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake, huku akiwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka vitendo vya uzembe na kuacha kuyapita magari mengine pasipo kuchukua tahadhari.



