*Ni la kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu sekta binafsi

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wahariri nchini washirikiane na Serikali kuelimisha wananchi ili kujenga mtazamo sahihi kuhusu umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi.

“Bado tuna kazi kubwa ya kujenga mtazamo sahihi kuhusu sekta binafsi. Bado kuna watu wanaoamini kwamba jambo likifanywa na sekta ya umma linaonekana kuwa la kizalendo, lakini likifanywa na sekta binafsi linaanza kutiliwa shaka kana kwamba kuna udanganyifu au wizi,” amesema na kuongeza:

“Mtazamo huo upo ndani ya Serikali, ndani ya sekta binafsi yenyewe na hata katika vyombo vya habari. Tunapaswa kuubadili. Hatutaweza kujenga uchumi wa nchi yetu kwa majira ya sasa bila kuwa na sekta binafsi imara.”

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Alhamisi, Novemba 26, 2026) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tisa wa Jukwaa la Wahariri (TEF) ulioanza leo katika Hoteli ya Morena, mkoani Morogoro na kusisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu ya kuelimisha wananchi kuhusu jambo hilo.

Akigusia kuhusu kaulimbiu yao isemayo: “Taaluma ya Habari Kujenga Umoja wa Kitaifa na Uchumi wa Vijana Kupitia Dira 2050,” Waziri Mkuu amesema hiuo ni kaulimbiu muafaka katika wakati muafaka. “Kaulimbiu yenu inagusa maeneo muhimu ya Taifa letu, yakiwemo taaluma ya habari, umoja wa kitaifa, uchumi wa vijana na utekelezaji wa Dira 2050.”

Amesema ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta binafsi ni ya umuhimu sana katika uzalishaji, uwekezaji na kuongeza ajira. “Kama kuna kazi ambazo sekta binafsi inaweza kuzifanya vizuri, tunapaswa kuweka mazingira mazuri ya kuifanya sekta hiyo ishiriki.”

Amesema kila mwaka kuna wahitimu wa ngazi mbalimbali wanaokadiriwa kuwa kati ya milioni 1.5 na milioni mbili ambao wote hawawezi kuajiriwa na Serikali. “Zamani kulikuwa na wahitimu wachache kiasi kwamba Serikali ingeweza kuwaajiri karibu wote. Hali ya sasa ni tofauti.

Akielezea umuhimu wa sekta hiyo, Waziri Mkuu amesema: “Lazima tujenge sekta binafsi itakayozalisha ajira, kuongeza uzalishaji na kuchangia mapato ya Serikali. Tunapaswa pia kuwa na wakandarasi wazawa wenye uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa ili fedha zinazotumika katika miradi ziendelee kuzunguka ndani ya uchumi wetu.”

Dkt. Mwigulu amewahimiza wahariri watumie vyombo vya habari kuimarisha umoja wa kitaifa, kupambana na rushwa na kuhimiza uwajibikaji katika jamii.

Mapema, Mwenyekiti wa TEF, Dkt. Deodatus Balile alisema Taifa lenye vyombo vya habari imara linaweza kupunguza gharama za kusimamia sheria, kukusanya kodi, kupambana na rushwa na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

“Mwananchi anapoelimishwa vizuri kuhusu wajibu wake wa kulipa kodi, hahitaji kulazimishwa kila wakati. Vyombo vya habari vinapochapisha habari za uchunguzi, vinaweza kusaidia kuokoa mabilioni ya shilingi yanayopotea kutokana na ubadhirifu na matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma,” alisema.

Alisema habari sahihi pia zinaweza kuzuia migogoro kabla haijasababisha madhara makubwa kwa maisha na rasilimali za Taifa na wao wanaamini kwamba kuwekeza katika vyombo vya habari ni kuwekeza katika utawala bora, amani na maendeleo ya Tanzania.

Dkt. Balile alisema TEF imejipanga kuanzisha programu ya kuwalea waandishi wa habari vijana kwa kutumia wahariri wakongwe na wastaafu. “Tunataka kujenga kizazi cha wanahabari kinachoweza kutofautisha habari zilizothibitishwa na taarifa zinazosambaa mitandaoni.”

“Tunatambua mchango wa mitandao ya kijamii katika kusambaza taarifa kwa haraka. Hata hivyo, tusipowekeza katika matumizi sahihi ya teknolojia, mitandao inaweza kutumiwa kuchochea chuki na migawanyiko badala ya kujenga Taifa. Tunataka kuwe na ushirikiano bora kati ya magazeti, redio, televisheni na mitandao ya kijamii katika kuzalisha na kusambaza habari zenye ubora,” alisisitiza.