Vyombo kadhaa vya habari vimeandika taarifa za Mjumbe wa Bodi ya African Parks Network (APN), James Lembeli, kuwashitaki wanahabari na wahariri wa vyombo kadhaa vya habari.

Kwenye orodha hiyo, jina la Manyerere Jackton limo. Pamoja nami, kuna makomredi wengine walioamua kwa haki kabisa kusimama kidete kulinda rasilimali za nchi yetu. Wito wangu kwa wote — tusikate tamaa.

Hadi naandika makala haya, sijapokea barua yoyote kutoka, ama kwa Lembeli au katika Mahakama ikinieleza bayana suala hilo. Kwa sababu hiyo, bado taarifa hizi nazichukulia kama taarifa nyingine zisizo rasmi, ingawa lisemwalo lipo, na kama halipo, laja.

Kama ni kweli Lembeli anakusudia kunishitaki mimi binafsi na wadau wengine, siwezi kumzuia. Ana haki na wajibu wa kufanya hivyo, hasa kama hisia zake na za marafiki zake zinamwaminisha kuwa hiyo ndiyo njia sahihi ya kuzima mwangwi wa vyombo vya habari na waandishi, walioamua kwa dhati kabisa kutetea na kulinda maslahi mapana ya kiuchumi ya Taifa letu.

Kuwapo kwa mpango wa kuikabidhi Hifadhi ya Katavi na hifadhi nyingine kwa APN siyo jambo la siri. Mpango huu unashinikizwa na Lembeli kwa kutumia kofia yake ya uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, na pia yeye kama Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa APN.

Kwenye magazeti, Lembeli amenukuliwa akitoa madai kadhaa. Miongoni mwa hayo anakana kwamba hajawahi kuzungumza na Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda juu ya utoaji wa Hifadhi, Mapori na Mbuga za Taifa kwa APN. Pili, anadai kwamba hakwenda Johannesburg, Afrika Kusini kushiriki mkutano wa Wizara ya Maliasili na Utalii na APN.

Lembeli ni kaka yangu. Lembeli kwa muonekano wake, na namna anavyoapa bungeni, ni muumini wa Mungu wa kweli. Haya yaliyoandikwa, kama kweli ni yake, hajamtendea haki Mungu wake.

Lembeli alikuwa mmoja wa watu waliokuwa kwenye mkutano wa Machi 27, 2014 uliofanyika Johannesburg. Mkutano huo ulipewa jina la “Mkutano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na African Parks Network”.  Kwa kimombo imeandikwa: “The Meeting between the Ministerial Delegation from Tanzania and the Top Management of African Parks Network”.

Kiongozi wa ujumbe huo wa “wizara” alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu. Pamoja nao, wengine waliohudhuria mkutano huo ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Paul Sarakikya; Mkurugenzi wa Utalii katika Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Ibrahim Mussa; Meneja Uhusiano wa TANAPA, Pascal Shelutete; na Katibu wa Waziri (Nyalandu), Imani Nkuwi.

Kwa upande wa APN waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa APN, Robert-Jan van Ogtrop; Mkurugenzi Mtendaji APN, Andrew Parker; Mkurugenzi wa Operesheni APN, Leon Lamprecht; na Meneja wa Miradi APN, Patricio Ndadzela.

Nauli za ndege na fedha za kujikimu kwa ujumbe huo zilitolewa na TANAPA kwa maelekezo ya Nyalandu. Kwa hiyo Lembeli anaposema hakwenda Afrika Kusini kwa shughuli hiyo, anadanganya.

Maandalizi ya safari hii na gharama zake yanatia shaka. Kuna mgongano mkubwa wa maslahi. Kama Lembeli si mtumishi katika Wizara ya Maliasili na Utalii, ilikuwaje akatajwa kuwa sehemu ya ujumbe wa “wizara?” Kama yeye si sehemu ya watumishi wa Wizara, ilikuwaje TANAPA wakachukua dhima ya kugharimia safari yake yote?

Kama Lembeli anadai kwamba alikwenda Afrika Kusini katika mkutano huo kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, kwanini Bunge lilijiweka kando kumlipia nauli na gharama nyingine?

Lembeli ni Mjumbe wa Bodi ya APN. Alikwenda Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa ushawishi wa APN kukabidhiwa Hifadhi, Mapori na Mbuga za Tanzania. Wakati huo huo alikuwa kwenye “delegation” ya Tanzania. Je, anaweza kueleza umma wa Watanzania, kwa dhati kabisa, kwenye mkutano huo alisimama kutetea maslahi ya upande upi?

Kwenye taarifa ya Sarakikya kuhusu mkutano huo, ya Machi 31, mwaka huu, anaeleza haya kwa kimombo: “The park/reserve under APN will retain all revenues. It was not shown how much should go to the government; say as percentage of gross annual income.” Kwa maneno mepesi ni kwamba hawa jamaa wanataka wahodhi mapato kwenye hifadhi au mapori watakayokabidhiwa. Wapo kwa faida zaidi. Je, Lembeli kama Mjumbe wa Bodi ya APN atakubali kutetea maslahi ya Tanzania, na kuacha maslahi yake na APN? Watanzania hawahitaji upako kutambua kuwa kwenye mzani huu Lembeli yupo upande wa APN.

Lakini si hivyo tu, bali kuna harufu nyingine ya ukoloni mamboleo ambayo kina Lembeli wanataka kuileta kwa lengo tu la kuwaweka kando Watanzania.

Kwenye ripoti iliyoandikwa na Sarakikya, ikieleza yaliyojiri kwenye mkutano huo, kwa kimombo, inasema: “Most existing staff are retained, but the non-performing staff are returned to the government. However, the top management for each park/reserve is appointed by APN including Chairman of the Board. It was not clear if remuneration and incentives of the staff will be better when APN takes over the management of the area.” Hapo kwenye wino mweusi ndipo kunakothibitisha hoja za wadau tunaopinga mpango huu ambao hauna tofauti na ule wa kinyonyaji wa umeme kutoka kwa kampuni ya Net Group Solutions ya huko huko Afrika Kusini.

Jambo la pili kama nilivyosema hapo juu, Lembeli anadai kwamba hajawahi kuzungumza na Waziri Mkuu juu ya ujio wa APN. Hapa anaudanganya umma. Kwenye barua ya Septemba 17, 2013 iliyoandikwa na Waziri Mkuu Pinda kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete, Lembeli anatajwa hivi: “Kikao hicho maalum kiliwahusisha  mawaziri (Maliasili na Utalii; na Mazingira), Wabunge (Mheshimiwa Lembeli na Dk. Kamani) na Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Madhumuni ya kikao hicho ilikuwa kukutana na mtaalamu wa asasi ya African Parks Network (APN) yenye makao yake nchini Afrika Kusini, Dk. Anthony Hall-Marton, inayosimamia Uhifadhi wa Wanyamapori katika Mbuga mbalimbali hapa Afrika.”

Lakini kabla ya hapo, Septemba 10, 2013 Waziri Mkuu alimwandikia barua Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Balozi Khamis Kagasheki, iliyokuwa na kichwa cha habari: “Semina ya Wabunge kuhusu ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kukuza uhifadhi endelevu wa wanyamapori katika maeneo ya hifadhi”.

Katika barua hiyo, Waziri Mkuu anamkumbusha Kagasheki kwa kusema, “Utakumbuka kwamba tarehe 11 Mei, 2013 niliitisha kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma ambacho ulihudhuria. Wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Mheshimiwa Dk. Charles Kitwanga, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira); Mheshimiwa James Lembeli, Mbunge wa Kahama na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira; na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii; na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu”.

Kwa maelezo haya mafupi, utaona kuwa Lembeli ameuhadaa umma. Ameuhadaa kwa sababu, mosi, alisafiri kwenda Afrika Kusini akiwa sehemu ya ujumbe wa “Wizara”. Pili, ameshamwaga ushawishi mwingi kwa Waziri Mkuu kuhusu hatua ya APN kukabidhiwa mapori na hifadhi za Taifa.

APN ni nani?

Pengine ni vema tukawajua hawa ni nani. APN ilianzishwa mwaka 2000. Makao yake yapo Afrika Kusini, Ni shirika lisilo la kiserikali linalosimamia na kuendesha hifadhi za taifa katika nchi saba barani Afrika.

Hifadhi hizo ni Akagera (Rwanda), Mjete (Malawi), Liuwa Plain na Bangweulu Wetlands (Zambia); na Garamba (DRC) na Odzala-Kokoua (Jamhuri ya Congo).

APN walikabidhiwa Hifadhi ya Taifa ya Nech-Sar na Omo nchi Ethiopia, lakini baadaye walifukuzwa.  Kadhalika, nchini Sudan walikabidhiwa Hifadhi ya Taifa, lakini Oktoba 2008 wakafukuzwa pia. Kwa kawaida wao hufanya kazi kwa kuingia mikataba na Serikali na hivyo hujitwalia mamlaka ya kuendesha maeneo yaliyohifadhiwa kibiashara.

Kwanini Katavi?

Lakini kwanini Katavi? Hifadhi ya Taifa Katavi ipo katika Mkoa wa Katavi ambako ni nyumbani kwa Waziri Mkuu Pinda. Lembeli, kwa ushawishi mkubwa, na kwa kutambua anaweza kufanikiwa kwa kuanzia kwa Waziri Mkuu, alihakikisha mpango huo wa APN unaanzia Katavi.

Katika barua ya A. Sang’enoi kwa niaba ya Waziri Mkuu ya Desemba 30, 2013 kwenda kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), ofisa huyo anamnukuu Rais Kikwete kwa kusema: “Waziri Mkuu aliwasilisha suala hili kwa Mheshimiwa Rais ambaye pamoja na kupongeza dhamira hii mpya na kuiunga mkono, aliagiza kuwa ichaguliwe maeneo ya kujaribia dhana hii (pilot area) ili mafanikio yake yasaidie kujenga imani kwa wadau na wananchi kwa ujumla.”

Kwa kutumia maneno hayo ya “kuchagua maeneo ya kujaribia”, Lembeli, na kwa namna ya kumvuta Waziri Mkuu ili awe naye bega kwa bega kubariki mpango huu wa kutoa hifadhi kwa APN, akawezesha mpango uanzie Katavi!

Turejee kwenye mada. Machi 18, mwaka huu, wataalamu walitoa taarifa yao juu ya hatari ya kuwakaribisha APN na asasi nyingine zenye maudhui kama yake, kusimamia na kuendesha sehemu za hifadhi.

Kikao kilianza Aprili 14-15, mwaka huu kikiwa ni kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu Pinda aliyoyatoa kwenye mkutano uliofanyika Dodoma mnamo Mei 11, 2013. Wataalamu waliounda jopo hilo walitoka TANAPA, TAWIRI, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mweka. Wataalamu hao walipitia mada ambazo ziliandaliwa kwa ajili ya kuwasilisha kwenye semina ya wadau kujadili mpango wa “APN” kama alivyoagiza Waziri Mkuu.

Ripoti hiyo ya wataalamu wazalendo iliainisha mambo mengi. Lembeli na Nyalandu wanayajua, lakini pengine kwa sababu wanazozijua, hawataki Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na hata Rais mwenyewe, wayajue. Hapa nitajitahidi kuyataja kwa ufupi.

Wataalamu walisema wazi kuwa sekta binafsi imejikita kwenye misingi ya uzalishaji wenye tija, yaani unaozingatia faida zaidi kuliko uhifadhi. Dhana hizi mbili zina utashi unaokinzana.

Walibainisha kuwa tayari Wizara ya Maliasili na Utalii inatekeleza dhana ya ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma ambako sekta binafsi zinaruhusiwa kuwekeza kwenye matumizi endelevu ya wanyamapori. Wakabaini kuwa maeneo mengi yana migogoro ikiwamo ya mipaka na matumizi ya rasilimali ya wanyamapori.

Wataalamu hao wakasema maeneo ya hifadhi, hasa Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba ni muhimu na nyeti kwa kuwa ni maeneo ya urithi wa asili wa pekee, yanayotumika kutunza rasilimali ya wanyamapori ambayo ni muhimu kitaifa na kimataifa.

Ikabainishwa kuwa usimamizi wa Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba ni suala mtambuka ambalo linahusisha sera na sheria za sekta nyingine — sekta ya ardhi, sekta ya kilimo, sekta ya mifugo na sekta ya mazingira.

Wakaona kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika masuala ya uhifadhi, hasa uhifadhi wa wanyamapori. Wakapongeza namna TANAPA, NCAA na Idara ya Wanyamapori wanavyosimamia maeneo yao, na kusema ni jambo la kujivunia mno.

Lakini kubwa katika hili, wataalamu wakabaini kuwa APN, sawa na wawekezaji wengine, haijawahi kuwasilisha maombi kuhusu kuruhusiwa kusimamia maeneo ya hifadhi nchini kulingana na sheria na taratibu za nchi.

Wataalamu hao wametumia maneno haya: “Ilipaswa kuiomba Serikali kwa maandishi kupitia Wizara husika, badala yake imetumia mbinu za ujanja ujanja na ‘lobbing’ ili kupatiwa maeneo ya hifadhi ya kusimamia kwa gharama ndogo sawa na bure bila masharti yoyote. Aidha, APN inapaswa kugharimia mchakato kuhusu mabadiliko haya ambayo inataka kuyaleta. Serikali haipaswi kugharimia suala ambalo haliko kwenye sera, sheria, mikakati yake na hata kwenye mpango kazi.”

Mapendekezo ya Wataalamu

Wataalamu hao wametoa mapendekezo kama wataalamu wasomi, lengo lao likiwa kuinusuru nchi dhidi ya hiki kinacholetwa na Lembeli kupitia APN.

Wanasema; “Serikali ishauriwe kwamba kwa sasa siyo njia mwafaka kushirikisha sekta binafsi katika kusimamia maeneo yaliyohifadhiwa kwa sababu sera na sheria imeweka jukumu hilo kwa Serikali na taasisi zake.

“Serikali itatue migogoro iliyopo kwanza kabla ya kuruhusu sekta binafsi, hususan APN kusimamia hifadhi na mapori ya akiba ambayo kwa sasa yamegawiwa kwa wawekezaji wengine kwa vipindi tofauti.

“Serikali na taasisi zake ziendelee kusimamia rasilimali ya wanyamapori na kuhakikisha kwamba zinahifadhiwa kwa maslahi ya Taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho.”

Timu hiyo ya wataalamu ilipendekeza majina ya kamati ndogo kutoka miongoni mwao ili wakutane kabla ya semina ya wadau kwa ajili ya kukamilisha mada na mawasiliano na kuandaa maelezo ya Waziri ambayo yangekuwa msimamo wa Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa dhana ya ushirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP). Wajumbe hao ni Selvanus Okudo (Idara ya Wanyamapori), Profesa Vedasto Ndibalema (SUA), Dk. James Wakibara (TANAPA) na Mabula Misungwi (Idara ya Wanyamapori). Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, semina hiyo ilikuwa haijafanyika.

Ni hatari kwa APN kukabidhiwa hifadhi na mapori ya akiba kwa sababu yenyewe inachojali ni faida zaidi ya uhifadhi. Ndiyo maana wataalamu wanashauri hivi: “APN wanashawishi kupatiwa maeneo ya Hifadhi ya Taifa na Mapori ya Akiba kwa kigezo kuwa Serikali imeshindwa na hivyo wao watayaboresha. Tunashauri, kwa sasa sekta binafsi iendelee kushiriki katika kuwezesha na kusaidia shughuli za uhifadhi na siyo kusimamia na kuendesha maeneo ya hifadhi hadi hapo uchambuzi wa kina kuhusu mgawanyo wa mapato, hatima ya watumishi na pia inapitia ya sera na sheria utakapokamilika ili kupata miongozo.

“Uhifadhi ni zaidi ya biashara kwa sababu thamani ya bioanuai ni zaidi ya pesa. Hivyo tunapendekeza kwamba Serikali itoe kipaumbele kwa mikataba inayotilia umuhimu uhifadhi badala ya biashara. PPP ni dhana ambayo Serikali inaitekeleza kupitia Sera na Sheria ya Ushirikiano ya mwaka 2009. Utekelezaji wa dhana hii bado uko katika hatua za awali hususan kwenye sekta ya wanyamapori, hivyo kwa sasa ni mapema mno kuanza kutumika katika kusimamia na kuendesha Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba kwa kuwa bado sekta ya umma haijashindwa. Hivyo, mabadiliko yoyote katika usimamizi wa maeneo hayo ni muhimu yazingatie mapitio ya sera na sheria,” wanasema wataalamu.

Maneno ya Katibu Mkuu Kiongozi

Kwenye suala hili la APN kukabidhiwa Hifadhi na Mapori, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, amekuwa makini kwa kutoa hadhari na maelekezo ya kisera na kisheria. Lakini, Waziri Mkuu Pinda anamuondoa shaka Rais Kikwete.

Katika barua yake ya Septemba 13, 2013 Pinda anamwambia Rais Kikwete: “Mjadala huu umekuja wakati Serikali imeanza kutekeleza Sera ya Taifa ya Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi ya mwaka 2009. Hivyo, suala hili halitakuwa na kipingamizi cha kisera.”

Katika barua ya Katibu Mkuu Kiongozi ya kwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii ya Oktoba 9, 2013, Sefue anaagiza: “Upembuzi uzingatie, pamoja na mambo mengine, changamoto ya ujangili, Sera na Sheria za Nchi, na mfumo wa kitaasisi uliopo ambao unaipa TANAPA mamlaka ya kuendesha hifadhi za wanyamapori. Aidha, faida na hasara za mfumo na uzoefu wa nchi nyingine uzingatiwe. Hakikisha unashirikiana na Wizara yenye dhamana ya uwekezaji katika kutekeleza hili.”

Kwa kauli hii, hofu ya Sefue iko wazi, nayo ni kwamba endapo APN au asasi nyingine za aina hiyo zitakabidhiwa dhima ya kuendesha hifadhi na mapori bila kufanyika kwa upembuzi, kunaweza kuibuka migongano mingi na hatari kwa uhifadhi nchini.

Maneno haya ya Katibu Mkuu Kiongozi yanawiana na msimamo wa wataalamu waliopitia ujio wa APN ambao wamesema wazi: “APN sawa na wawekezaji wengine haijawahi kuwasilisha maombi kuhusu kuruhusiwa kusimamia maeneo ya hifadhi nchini kulingana na sheria na taratibu za nchi…ilitumia mbinu za ujanja ujanja na lobbying ili kupatiwa maeneo.”

Haya nimethubutu kuyaweka wazi ili wasomaji watambue kuwa tunaposhughulikia masuala yenye maslahi ya Watanzania, hatufanyi hilo kwa hila wala husda. Hakuna aliye tayari kumvunjia heshima Lembeli wala mtu yeyote mwenye nia njema na rasilimali zetu. Tuna haki na wajibu wa kuhoji dhamira na maudhui ya viongozi wetu. Kiongozi wa umma lazima awe tayari kuhojiwa na kutoa majibu yanayoridhisha, na si kwenda kuisumbua Mahakama ambayo imejijengea heshima kubwa.

Tunahoji uhalali wa APN kwa sababu kimtazamo hii ni aina nyingine ya ukoloni mamboleo inayoletwa na raia wa Afrika Kusini. Nchini mwao hakuna Hifadhi ya Taifa kwa maana ya maneno hayo. Huko kuna hifadhi za watu binafsi. Ndiyo maana wakati fulani wawekezaji fulani kule Serengeti walitumia maneno “Private Park” kuonesha kuwa eneo hilo ni mali yao! Waziri Shamsa Mwangunga alidhibiti uhuni huo. Hifadhi za Tanzania ni mali ya Watanzania. Mdhamini wake mkuu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lembeli ana mgongano wa maslahi katika suala hili. Hawezi kuwa Mjumbe wa Bodi ya APN halafu alinde maslahi ya Watanzania kupitia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Akili ya kawaida inawafanya wengi waamini kuwa alipewa ujumbe wa Bodi ili kupitia nafasi yake bungeni, na ukaribu wake na wakubwa serikalini, aweze kuhakikisha APN si tu wanapewa mapori, bali wanapewa hifadhi ambazo ni bora kabisa duniani.

Kulithibitisha hilo, ndiyo maana kwenye vikao vikubwa vinavyojadili ujio wa APN, amekuwa akihudhuria mwenyewe — na si kumtuma mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge anayoiongoza. Hamtumi mwingine kwa sababu hapo anatetea maslahi yake binafsi. Maslahi binafsi lazima umtume unayemwamini. Katika mgongano huu wa maslahi, Lembeli anatetea upande upi? Awe mkweli tu.

Lakini jambo linalotia shaka ni hatua ya Waziri Mkuu na wakubwa wengine kushindwa kumbana Lembeli kwenye suala hili ili kuondoa huu mgongano wa maslahi. Je, ni kweli kwamba Waziri Mkuu hajui kama Lembeli ni Mjumbe wa Bodi ya APN na wakati huo huo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira?

Je, Waziri Mkuu na wakubwa wengine, hawawezi kuhoji kwenye mlolongo huu wa vyeo vya Lembeli, atatetea upande gani?

Je, ina maana Waziri Mkuu na wakubwa wengine Ikulu, hawajatambua kuwa APN inakuja kimaslahi zaidi, na kwa sababu hiyo Lembeli hawezi kujiegemeza upande wa “kukosa?” ambao ndiko waliko Watanzania wengi?

Waziri Mkuu anashindwa nini kuhoji matumizi ya fedha za TANAPA — fedha za umma — kumsafirisha Mjumbe wa Bodi ya APN anayekwenda kutetea “ugali wake na familia yake?” Kwa safari hiyo, value for money iko wapi?

Watoto wetu wanaoketi chini wamekosa madawati mangapi kwa TANAPA kumlipia Lembeli? Ukijiuliza mengi unaweza kufikia hitimisho moja; nalo ni kwamba Lembeli amejijenga sana kwa wakubwa hawa, na kwa sababhu hiyo anataka kuwazima wanahabari wanaohoji na kudadisi hatima ya rasilimali za nchi yetu. Gharama ya urafiki wa Lembeli na Nyalandu kwa Taifa letu ni kubwa. Nashukuru nimeyasema haya. Akibisha, nitarejea hapa hapa.

By Jamhuri