*Kipande adai fidia Sh bilioni 5.85, aomba lizuiwe kuiandika Bandari

*Mahakama yasitisha kumfukuza Mkurugenzi, Njowoka kushitakiwa

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mzee Madeni Kipande (58) na mtu aliyejiita Katibu wa Shirika la TPA, Christian Chiduga, kwa pamoja wamelifungulia kesi Gazeti Jamhuri mahakamani na Mhariri Mtendaji, Deodatus Balile, wakidai fidia ya Sh bilioni 5.85.

Pia wawili hao walifungua kesi nyingine Mahakama Kuu chini ya Hati ya Dharura mbele ya Jaji Sheikh iliyotarajiwa kuitishwa Jumatatu jana, wakiomba Mahakama itoe amri ya zuio kwa JAMHURI isiendelee kuandika habari zinazohusu Bandari.

Katika hati hiyo, iliyoandaliwa na wakili Mpare Mpoki kama wakili wa walalamikaji, wanasema katika maisha yao hawajawajapata kuona gazeti linafuatilia habari moja kwa muda mrefu na mfululizo kama JAMHURI ilivyofanya kwa Bandari.

Wanasema habari zote zilizochapishwa ilikuwa kashifa kwao na Bandari imepoteza wateja kutokana na habari hizo zinazoeleza hatari inayoinyemelea Bandari kuwa kwa muda mrefu sasa haina CCTV Camera na taarifa zilizotolewa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyeonyesha kuwa bandarini kuna ubabe na matumizi mabaya ya madaraka.

Hadi tunakwenda mitamboni, Mahakama ilikuwa haijatolea uamuzi ombi la Bandari kutaka Gazeti Jamhuri lizuiwe kuendelea kuchapisha habari za Bandari. Gazeti hili limeamua kuchukua mkondo wa kisheria na litakujulisha msomaji hatua kwa hatua kinachoendelea.

Wakati huo huo, habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinasema Mahakama ya Kazi imemzuia Mzee Kipande na Bodi ya Wakurugenzi ya TPA kumfukuza kazi Mkurugenzi wa Masoko, Franciscas Muindi. Jana ilikuwa siku ya kusikiliza kesi hiyo ambapo Bandari walipaswa kujieleza kwanini wanataka kumfukuza kazi. Hadi tunakwenda mitamboni uamuzi ulikuwa haujatolewa. Mama Muindi amesimamishwa kazi na Mzee Kipande.

Katika hatua nyingine, wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari Tanzania (DOWUTA), wako mbioni kwenda mahakamani kushinikiza kufanyika kwa uchaguzi ndani ya chama hicho.

Wanachama hao kutoka Matawi ya Mwanza, Dar es Salaam na Mtwara wamefikia hatua hiyo baada ya Uongozi wa DOWUTA Taifa  kusitisha kufanyika kwa uchaguzi wa cahama hicho mwaka jana.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya chama hicho kimeieleza JAMHURI kwamba uamuzi huo utafikiwa leo baada ya kupata majibu kutoka kwa Msajiri wa Vyama.

“Tunatarajia kumuona Msajili kwa mara ya mwisho siku ya Jumanne (leo), akitupa majibu ya yasiyoridhirisha muda huo huo tunakwenda kwa mwanasheria wetu na kitakachofuata ni kwenda mahakamani,” amesema mtoa habari.

Amesema tayari wanachama katika matawi ya Mwanza, Mtwara na Dar es Salaam wamefikia mwafaka wa kwenda mahakamani kuushinikiza uongozi huo kufanya uchanguzi.

Amesema uongozi wa DOWUTA ulipo sasa umeshindwa kuwasaidia wafanyakazi, badala yake umekuwa upande wa manejimenti, na katika kipindi cha miaka mitatu umeshindwa kuwatetea wafanyakazi.

Moja ya malalamiko ya wafanyakazi hao ni kwamba Njowoka ameshindwa kuwatetea wafanyakazi kupata sare za kazi.

“Yaliyosemwa na Edmund Njowoka  kwamba kuna ari kubwa ya kufanya kazi si kweli ni aibu. Kuna wafanyakazi sare zao zimeshonwa viraka na hakuna dalidali zozote zinazoonesha kuwa tutapatiwa,” amesema.

Amesema pamoja na Bandari kutoa fedha za kujikimu katika mazingira magumu  ya kazi, chakula na usafiri, lakini Njowoka kwa kujipendekeza kwa uongozi wa juu alizuia fedha ya bonasi.

Amesema kwamba fedha hizo tayari zimepitishwa na Baraza la Majadiliano la Bandari (CJIC) kuridhia kutolewa kwa bonasi ya wafanyakazi na pia ilipitishwa na Hazina, lakini kutokana na maneno ya uchochezi yaliyopelekwa kwa uongozi na Njowoka imeshindikana kupata posho hiyo.

“Kulikuwa na kikao na Waziri, Dk. Harrison Mwakyembe, na uongozi ulitamka kuwa posho hiyo ingetoka mwezi wa Septemba mwaka jana, lakini hadi sasa posho hiyo haijatoka, hadi ninavyozungumza na wewe hapa hii yote ni kwa sababu ya Njowoka,” amesema.

Amesema kwamba CJIC na manejimenti walikubaliana na kuongeza mshahara kwa wafanyakazi kwa asilimia 11, lakini suala hilo lilipofika kwa Waziri Mwakyembe limekwama.

Amesema kwamba mambo hayo yanakwamishwa na Mwenyekiti wa DOWUTA ambaye kwa muda wote amekuwa akiudanyanga uongozi wa Banadari na Waziri Mwakyembe.

Katika barua waliyomuandikia Msajili wa Vyama ya Aprili 4, mwaka huu wanachma hao wameeleza kwamba wameshtushwa na kusikitishwa na waraka uliotolewa na Katibu Mkuu wa DOWUTA Taifa wa Machi 28, mwaka huu.

Waraka huo wenye kumbu namba Vol 1/10/14  ulihusika na kusogezwa mbele kwa Uchaguzi Mkuu. “Sisi wanachama wa DOWUTA Bandari ya Dar es Salaam huongozwa na Katiba na kanuni toleo la 2008, kwa kuwa tunaheshimu katiba na kanuni zinazotuongoza imetubidi tulete malalamiko yetu kwako msajili tukiamini kwamba wewe ndiye chombo cha kutupatia ufumbuzi wa haraka ili kuepuka matatizo yanayoweza kutokea kwenye chama na tasisi kwa ujumla.

“Ikimbukwe kamba uchaguzi  wa viongozi ulifanyika tarehe 17 Machi, 2009 na kusababisha kutupatia viongozi imara waliotuongoza hadi kumaliza muda wao wa uongozi wa miaka mitano mnamo tarehe 17 Machi, 2014 kwa mujibu wa katiba.

“Jambo la kustaajabu na kusikitisha na ambalo ni kinyume kabisa wamejiongezea muda wa mwaka mmoja bila ridhaa ya wanachama na kusababisha kuvunja katiba na kanuni zinazotuongoza, bila kujali kiapo cha kutii katiba ambayo imekuwa ikitumika kuongoza chama chetu.

“Ukitazama kipengele cha 14.0 kamati ya marekebisho ya katiba na kanuni ya 14.1, kazi na wajibu wa kamati itakuwa ifuatavyo:- 14.1.1 kupokea na kundaa mapendekezo ya marekebisho ya katiba na kanuni kutoka kwa wanachama.

“Kipengele namba 5.5 muda wa uongozi aya ya 5.5.1 uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali na wajumbe wa vikao vya chama utafanyika kwa mujibu wa katiba na mwaka kuzingatia kalenda ya uchaguzi na utaratibu unaoanishwa katika kanuni hii, hawa wote wanakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano.

“Pia tukinukuu katiba ya chama kipengele cha 6.3 muda wa uongozi 6.3.1, viongozi wote wa chama watakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano.

“Kwa kuwa chama kina katiba yake bado hatuoni sababu ya kufuata kalenda ya TUCTA kama ambavyo Katibu Mkuu wa DOWUTA Taifa alivyojieleza kwenye waraka wake uliokwishatajwa hapo juu, kwani wajumbe watakapokwenda kupiga kura wajumbe ambao wanachama watapata ridhaa kwa kuwachagua kwa kura halali katika uchaguzi halali na kwa kalenda ya uchaguzi halali wa kikatiba.

“Uchaguzi ni suala la kikatiba, hivyo kuzidisha muda wa uongozi na kujiamulia kuahirisha uchaguzi ni ukiukwaji mkubwa wa katiba ya chama na hapa tunapata swali la kujiuliza ya kwamba nguvu na ridhaa ya kujiongezea, muda wa kuendelea kuwepo madarakani wameipata wapi na kwa nani?

“Msajili, tawi lilikuwa lifanye mkutano mkuu kwa ajili ya kupitisha bajeti ya mwaka mpya wa fedha tangu Desemba 2013, lakini cha kushangaza na kusikitisha hadi leo tunapoandika hii barua hakuna mkutano wowote ulioitishwa na matumizi ya pesa za wanachama yanafanyika kama wanavyokata.

“Je, matumizi hayo ya fedha za wanachama yamepitishwa na nani, huu ni utaratibu mbaya  wa ukiukwaji na uvunjaji wa katiba ya chama chetu ambacho kimekuwa kikituongoza vizuri sana huko nyuma.

“Tunaamini kuwa kwa kuwa sababu iliyotolewa ya maandalizi ya katiba mpya bado haijawa tayari basi busara itumike ili katiba iliyopo iweze kupewa heshima yake na kuwashirikisha wanachama.

“Na hapo tunatoa rai pia ya kuhusishwa kwa wanachama walio wengi katika mchakato huo wa mabadiliko ya katiba ili mabadiliko hayo yasiwe ya upande mmoja tu wa viongozi walio wachache.

“Hivyo, kwa kumaliza tunaomba ofisi yako ilishughulikie suala hili mapema iwezekanavyo ili kulinda maslahi ya wanachama, chama chenyewe na taasisi zake kwa ujumla.

“Tunatumia nafasi hii pia kutoa angalizo kuwa ujanja unaotaka kutumika wa kusogeza muda wa uchaguzi hadi mwaka 2015 tumeubaini kwani nia yao ni kukaa hadi mwaka 2016 kutokana na kwamba mwaka 2015 kuna Uchaguzi Mkuu wa Taifa na hivyo, kuna uwezekano uchaguzi mwingine mdogo mdogo ukiwemo wa vyama vya wafanyakazi ukasimamama ili kupisha uchaguzi mkuu kufanyika kwa amani.”

Akijibu barua hiyo, Masajili wa Vyama na Waajiri, D. Uiso, ameitaka DOWUTA kuzingatia katiba ya chama hicho.

“Katiba ya DOWUTA toleo mwaka 2008 ibara ya 6.3.1 inazungumza kuwa muda wa viongozi kuwepo madarakani ni miaka mitano, kwa mujibu wa kumbukumbu za Ofisi ya Msajili uchaguzi wa miwisho wa matawi ulifanyika Machi 2009.

“Ni dhahiri kuwa uchaguzi mwingine unapaswa kufanyika ndani ya kipindi cha miaka mitano, yaani mwanzoni mwa mwaka 2014, maelekezo yoyote nje ya katiba hayawezi kuwa na nguzu kama hayana ridhaa ya wanachma,” amesema.

Uiso amewataka DOWUTA kuwasilisha ushahidi iwapo kulikuwa na kikao cha kikatiba kilichoidhinisha kuahirishwa kwa uchaguzi hadi mwaka 2015.

Amesema si vema chama hicho kuingia katika migogoro isiyo ya lazima. Aidha, kama kweli kulikuwa na maelekezo ya shirikisho wanachama wangefahamishwa kabla ya kuandaa waraka na sababu za maelekezo hayo kwa kuwa hivi ni vyombo viwili tofauti.

Hata hivyo, Msajili ametaka kuzingatia maelekezo ya katiba ili kuendeleza kukijeanga cahama hicho ambacho kimeakuwa kikieandelea vizuri

By Jamhuri