Panga kuvunja rekodi 

Kuna baadhi ya watu wanapopata matatizo wanavunjika moyo, wengine wanavunja rekodi. Kuwa na maono ya kuvunja rekodi katika eneo ulipo. Hakikisha viwango na masharti vinazingatiwa. Matendo yawe yanayokubalika kisheria na ni mema.  

Jiwekee viwango ambavyo vitakusaidia katika lengo lako la kuvunja rekodi. Akushindaye kwa kusema, mshinde kwa kunyamaza, vunja rekodi ya ukimya. 

Vunja rekodi ya mapato yako ya mwaka jana. Vunja rekodi ya vitabu ulivyovisoma mwaka jana. Vunja rekodi ya muda wako kwa mwaka wa kukaa kanisani siku ya Bwana. Vunja rekodi ya kukaa na wanafamilia wako. Vunja rekodi ya kuwa muungwana unaposafiri.  Vunja rekodi ya kubana matumizi. Vunja rekodi ya sala zako. 

Vunja rekodi ya matendo yako ya upendo. Vunja rekodi yako ya ukarimu. Vunja rekodi yako ya kutenda mema. Kama wewe ni mwandishi wa vitabu, vunja rekodi ya vitabu ulivyoviandika mwaka jana.

Ingia katika kundi la kizazi kinachoamini katika kuvunja rekodi. “Naamini watu wa vizazi vijavyo watakimbia haraka sana kwa sababu, utakavyoona, tunakimbia vizuri zaidi ya watangulizi wetu,” alisema Tirunesh Dibaba, Muethiopia anayeshikilia rekodi ya dunia ya meta 5,000. 

Ana umri wa miaka 28. Alizaliwa Februari 8, 1991. Kwa upande wa wanaume, rekodi ya dunia ya meta 5,000 inashikiliwa na Muethiopia Kenenisa Bekele kwa muda wa 12:37.35 na Tirunesh Dibaba kwa upande wa wanawake akiwa na muda wa 14:11.15. Wote wanatokea Ethiopia. 

Kuna mambo mbalimbali ya kutusaidia kuvunja rekodi. Kwanza, maandalizi; Wakenya wengi wanaokimbia kwa mwendo wa kasi wanatoka Bonde la Ufa. Wakiwa watoto wanatembea na kukimbia kwenda shuleni. 

Bahati humwendea mtu anayejiandaa. Maandalizi ni vijilia ya kuvunja rekodi. Pili, ni kuvunja hofu. “Huwezi kuvunja rekodi bila kuvunja hofu kwanza,” alisema Matshona Dhliwayo. Hofu ni adui namba moja wa kuvunja rekodi.

Tatu, shindana na nafsi yako. “Kuwa bingwa shindana; kuwa bingwa mkubwa shindana na watu wazuri sana; kuwa bingwa mkubwa sana shindana na nafsi yako,” alisema Matshona Dhliwayo. Shinda rekodi zako za mwaka jana katika nyanja mbalimbali: afya, elimu, miradi, kutaja maeneo machache.

Nne, ukiona lisiloonekana utafanya  lisilowezekana. “Mtu ambaye hapigi picha hana mbawa,” alisema Muhammad Ali. Piga picha ya rekodi yako mpya. Ona unavunja rekodi.

Tano, kuwa na mtazamo chanya. Watu wenye mtazamo chanya wanaona zawadi katika matatizo, wanaona fursa katika magumu. Wavunja rekodi ni watu wenye mtazamo chanya. Sita, kunahitajika moyo wa kuthubutu. Wavunja rekodi wana moyo wa kuthubutu.

Katika Biblia tuna mfano wa kuvunja rekodi na kubadilika kimaadili dakika za lalasama. Mualifu mwingine alisema: “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.” Yesu akamjibu: “Nakuambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.” (Luka 23:41-42). 

“Mwizi mwema” au “Mwizi aliyetubu” aliyetundikwa na Yesu msalabani alivunja rekodi dakika za lalasalma. Alitubu. Huyu alikuwa upande wa kulia wa Yesu, kwa vile shingo ya Yesu msalabani inachorwa ikiangukia mkono wa kulia. Anaitwa Dismas. Katika Kanisa Katoliki kuna siku ya kumkumbuka tarehe 25 Machi kama Mtakatifu Dismas. Lakini bahati ya mwenzako isikulaze mlango wazi. Tenda mema. Usiseme: “Nitakuwa kama mwizi aliyeiba mbingu.” Kadiri ya Yohane Krisostomu, mwizi huyu alikaa jangwani na kuiba au kuua mtu yeyote asiye na bahati akivuka njia yake. Kadiri ya Papa Gregori I alikuwa na hatia ya damu na hata damu ya ndugu yake.  Alivunja rekodi ya kubadilika katika maisha yake. Vunja rekodi ya kubadilika na kuwa mwema.

By Jamhuri