Home Makala Ubalozi wa China chachu ya maendeleo ya elimu nchini

Ubalozi wa China chachu ya maendeleo ya elimu nchini

by Jamhuri

Ubalozi wa China nchini Tanzania umeendelea kutoa msaada kwenye maendeleo ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na kuchangia ujenzi wa shule na kutoa elimu ya lugha ya Kichina ambayo imekuwa ikifundishwa katika shule na vyuo mbalimbali nchini.

Wiki iliyopita Ubalozi wa China nchini uliwatunuku wanafunzi 80 kutokana na matokeo mazuri katika lugha ya Kichina. 

Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke, amesema China itaendelea kutoa msaada kwenye maendeleo ya elimu nchini Tanzania.

Amesema anatumaini kuwa tuzo walizopewa wanafunzi hao zitawahimiza wanafunzi wengi zaidi kujifunza lugha ya Kichina na kupata udhamini wa masomo unaotolewa na Serikali ya China ili kujifunza lugha ya Kichina nchini China siku zijazo.

Balozi Wang amebainisha kuwa idadi ya wanafunzi wa lugha ya Kichina imeongezeka na kufikia 17,000 nchini Tanzania, wakifundishwa na walimu 80.

Ili kuendeleza ushirikiano wa Serikali ya China na Tanzania, China ni nchi kinara inayotoa ufadhili kwa idadi kubwa ya wanafunzi wa Tanzania wanaoomba ufadhili wa kusomea kozi mbalimbali nchini humo. 

Balozi Wang amesema kwa mwaka huu, Serikali ya China imetoa nafasi 302 za ufadhili kwa wanafunzi wanaojifunza kozi mbalimbali nchini.

Amesema kuwa Serikali ya China imekuwa nchi inayotoa idadi kubwa zaidi ya nafasi za ufadhili kwa wanafunzi wa Tanzania. 

“Wanafunzi 1,900 wamepata ufadhili wa Serikali ya China na kwenda kusoma nchini China, miongoni mwao wamehitimu na wamerudi Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa taifa lao katika sekta mbalimbali,” amesema Wang.

Katika tuzo hizo, wanafunzi 20 wamepata tuzo bora na wengine 60 wamepata tuzo ya mafanikio, wanafunzi hao ni kutoka vyuo mbalimbali nchini. 

Katika hafla hiyo, mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Teknolojia, Ole Nasha, ambaye amesema kwamba, ushirikiano wa China na Tanzania ni wa kihistoria, ambao matokeo yake ni pamoja na  ujenzi wa Reli ya TAZARA.

“Tunao vijana wengi ambao wanasoma kwenye vyuo mbalimbali kwa msaada wa Serikali ya China, tutambue kuwa China imekuwa sehemu ya wanafunzi wa Kitanzania kwenda kujipatia mafunzo mbalimbali,” amesema Ole Nasha. 

Kwa kipindi cha miaka mitatu, Ubalozi wa China nchini umeweza kutoa ufadhili wa wanafunzi 200 kwenda nchini China masomoni. 

Baadhi ya wanafunzi waliopata tuzo bora za mafanikio wameeleza kuwa lugha ya Kichina ni lugha iliyo sokoni kwa sasa, hivyo ni muhimu lugha hiyo kuzingatiwa kutokana na ubora wake pamoja na kukua kwa sayansi na teknolojia. 

“Lugha ya Kichina kwa sasa ipo sokoni, kwa Mtanzania kujua lugha mbalimbali duniani zitamsaidia kupata ajira hata kwenye makampuni ambayo yanatoa ajira kwa kuzingatia kigezo cha kujua lugha yao,” amesema. 

Novemba mwaka jana Serikali ya China ilisaini mkataba wa ujenzi wa chuo cha kisasa cha mafunzo ya ufundi stadi (Veta) mkoani Kagera kinachogharimu Sh bilioni 22.4. Fedha hizo zimetolewa na Serikali ya China katika kusaidia elimu ya ufundi nchini.

Chuo hicho cha kitaifa cha Veta kimejengwa kwenye kiwanja chenye ukubwa wa hekta 26,000 kilichopo eneo la Kahororo, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.

You may also like