Kujifunza huanza pale woga unapokufa

Woga ni adui wa vingi. Woga umefanya watu wengi wafe na wazikwe wakiwa na vitu vya thamani ambavyo dunia ilihitaji kufaidika navyo lakini kilichofaidika ni udongo. Woga umezaa umaskini, woga umefanya watu wakose haki zao. Hayo ni baadhi ya matokeo ya woga.

Katika kujifunza nimegundua pia kwamba woga ni adui namba moja. Tunashindwa kujifunza vitu vingi na vyenye manufaa kwetu kwa sababu tunatanguliza woga mbele yetu. Kujifunza huanza pale woga unapokufa.

Ukitaka kuwa mtaalamu au mbobezi katika kitu fulani sharti weka woga pembeni. Kwenye kanuni za mafanikio neno woga halimo bali kuna neno ujasiri.

Nataka nikupe mfano ulio wazi kabisa. Watu wengi tumekulia katika jamii ambazo tuliamini kwamba somo la Hesabu ni janga la taifa (mimi pia nimekulia katika jamii ya namna hiyo). Kilichojificha nyuma ya dhana hii ni woga, si woga tu bali woga wa kurithishana, kizazi kimoja kwenda kingine, mtaa mmoja kwenda mwingine, mpaka inafikia hatua taifa zima tunasema: “Hesabu ni janga la taifa.”

Je, kurithishana huku kukoje? Jambo hili hutokea pale ambapo mtu hata kabla hajaanza kusoma Hesabu tayari anaambiwa: “Hesabu ni ngumu mno.” Mtu huyu anatengeneza kitu kichwani ambacho mwisho wa siku hata akiwa darasani hawezi kutulia na kusikiliza kile mwalimu anachofundisha kwa sababu kichwani mwake maneno yanazozunguka ni haya: “Hesabu ni ngumu sana, Hesabu ni janga la taifa.” Si rahisi mtu kama huyo kufaulu Hesabu kwa sababu tayari kuna woga amekwisha kuutengeneza.

Hakuna anayejifunza kitu na kukifahamu hapo hapo, kama wapo ni wachache. Nilipokuwa kidato cha kwanza mwalimu wangu mmoja aliniambia msemo mmoja wa Kilatini ninaoukumbuka siku zote, alisema: “Repetitio est mater studiorum,” akimaanisha: “Marudio ni mama wa masomo/kujifunza.” Kila unayemuona ni mbobezi katika sekta fulani kuna siku alikuwa mpya katika sekta hiyo, lakini huo haukuwa mwisho wake aliamua kuanza kujifunza na hatimaye kuwa mbobezi.

Ni katika kurudia mara nyingi tunapobobea katika kile tunachojifunza. Kumbe inawezekana kuna wengi walishindwa maswali matano wakiwa shule ya msingi na hadi leo wanaamini kwamba kwao Hesabu ni mtihani, yaani kwamba somo la Hesabu limeshindikana. Woga mkubwa bado umewatawala.

Ukitaka kujifunza kitu kwenye maneno yako ondoa maneno kama: “Ninavyojijua sitaweza.” “Watu watanionaje?” “Haya ni mambo magumu.”

Kadiri unavyojitajia maneno ya kutoweza unakuwa unaupa woga nafasi kubwa ya kutawala kile unachokifanya. Woga unapotawala hauwezi tena kujifunza.  

Ben Carson, si jina geni katika masikio ya wengi. Huyu ni daktari maarufu wa  ubongo, ni daktari wa kwanza aliyefanya upasuaji wa kutenganisha watoto waliozaliwa vichwa vyao vikiwa vimeungana.

Historia ya Ben Carson inasisimua kidogo. Kwanza walilelewa na mama yao yeye na kaka yake aliyeitwa Curtis, hii ilikuwa ni baada ya baba yao kuitelekeza familia. Mama yao alikuwa akifanya kazi kama mfanyakazi wa ndani kwenye nyumba za matajiri.

Ben alikuwa ni mwanafunzi aliyezoea kushika mkia darasani, matokeo yake yalijaa namba za viatu, tena inawezekana viatu vya watoto. Mama yake katika nyumba zile alizofanya kazi aligundua kitu kimoja, familia za matajiri wanasoma sana vitabu. Hivyo aliwaamuru watoto wake kutotazama televisheni na kuanza tabia mpya kusoma vitabu.

Ilimpasa kila mtu kusoma vitabu visivyopungua viwili kila wiki. Kazi haikuishia hapo, walipaswa kutoa mrejesho wa kile walichokisoma katika vitabu hivyo mbele ya mama yao. Zoezi hilo walilifanya kila mwisho wa wiki, ingawa baadaye ilikuja kugundulika kwamba mama yao alikuwa hajui kusoma.

Siku moja mwalimu akiwa darasani alishika jiwe dogo akauliza: “Nani anafahamu tabia za jiwe hili?” Darasa zima mikono chini. Ghafla mkono ukaonekana nyuma, darasa zima likageuka kutazama ni nani huyu anayejua jibu hilo. Alikuwa ni Ben aliyeshika namba za mwisho. Ben akasimama na kutaja tabia za jiwe lile. Mwalimu wake akastaajabu kwakuwa alipatia. Toka siku hiyo darasa lake likaacha kumdharau, wanafunzi wenzake walikuwa hata hawachezi naye kwani walijua hana akili.

Tangu siku hiyo ufaulu wake ukaanza kupanda darasani, akaanza kushika nafasi za juu. Alifanya hivyo mpaka chuo kikuu mpaka akawa daktari bingwa duniani. Huyu aliamua kuua woga ndani yake na kuanza kujifunza.  

By Jamhuri