Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

IMEELEZWA kuwa wakati wa mabadiliko ya sheria zinazominya uhuru wa habari nchini ni sasa na kwamba, harakati za kudai mabadiliko ya sheria hizo ilianza siku moja baada ya sheria zilizopo sasa kusainiwa mwaka 2016 na kuanza kutumika.

Hayo yameelezwa na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Neville Meena wakati akizungumza na Kituo cha Radio cha Dodoma (Dodoma FM) leo Agosti 22,2022

“Awali serikali haikuonesha dhamira ya kushughulikua maoni ya wadau wa habari nchini, lakini katika utawala huu wa Serikali nayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan dhamira imeoneshwa tangu mwanzo, tunaamini tutafanikiwa,’’ amesema Meena.

Amesema,Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 iliacha mambo ya msingi katika kukuza tasnia ya habari na badala yake, sheria ambazo ni ngumu kutekelezwa.

Na kwamba, kutokana na kuwepo kwa mazingira magumu ya habari na wanahabari nchini, tasnia ya habari iliyumba kwa kiwango kikubwa.

“Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipingwa na wadau wa habari siku moja baada ya kupitishwa ili kutumikaa. Si kwamba, hakukuwa na vitu muhimu kwa wanahabari, wadau waliona imebeba mitego na madhara mengi kwa wanahabari na vyombo vya habari,’’ amesema Meena

Amesema kuwa kuna lawama zinaelekezwa kwa vyombo vya habari kukosa weledi, moja ya changamoto inayovikabili ni kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati.

Vinashindwa kulipa mishahara kwa kuwa, watangazaji wengi hasa Serikali kwenye halmashauri,wanatoa matangazo lakini hawataki kulipa hivyo kuchangia kushuka kwa weledi kwenye vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari vinalalamikiwa kukosa weledi, lakini tukumbuke kwamba wanaotoa matangazo na kushindwa kulipa, wanachangia kutengeneza tatizo.

“Wanaoongoza kutolipa ni wakurugenzi wa halmashauri, hili linachangia kuyumbisha vyombo vya habari na ndio maana tumependekeza baada ya miezi sita mtangazaji kushindwa kulipa, licha ya kukumbushwa basi afikishwe mahakamani,’’ amesema.

Pia amesema, ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka wadau wa habari wakutane na kuchakata mapendekezo ya sheria za habari, imetimia.

“Suala la mapendekezo yote ya wadau wa habari kupita, hilo ni suala lingine. Cha msingi ni kwamba, miongoni mwa ahadi za Rais (Samia), ikiwemo wizara kukutana na wadau wa habari na kupitia vifungu, imetekelezwa.

“Sisi kama wadau wa habari tunaamini tunakwenda kufanikiwa kwa kuwa, hata Waziri Nape (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) ana hisia chanya katika mchakato huo,’’ amesema.

Amesema, miongoni mwa mapendekezo ya wadau wa habari katika mabadiliko ya sheria za habari nchini, ni kuwa uamuzi wa mahakama uwe unaheshimiwa.

Amesema, baadhi ya vyombo vya habari licha ya kushinda kesi mahakamani lakini kumaliza vifungo vyao, Idara ya Habari Malelezo iligoma kuwapa leseni ili kuendelea na upashaji habai.

“Kuna gazeti (MwanaHalisi) licha ya kushinda kesi mahakamani, hawakupewa leseni ya kuendelea na uchapaji habari. Hao hao pia hata walipomaza kifungo bado hawakupewa leseni, jambo hili sio sawa hata kidogo,’’ amesema Meena.

Amesema, wadau wa habari nchini wamependekeza kwamba, mahakama inapotoa hukumu juu ya jambo fulani, basi serikali inapaswa kutekeleza kinyume na ilivyo sasa.

“Mkurugenzi wa Habari Maelezo anatumia sheria ile ile ambayo sasa inalalamikiwa ya kuwa na uamuzi wa kutoa leseni kwa chombo cha habari ama kutotoa kwa utashi wake.

“Katika hili tunapendekeza gazeti likishasajiliwa basi liendelee na kazi kwa kufuata taratibu zilizopo. Unapofunga chombo cha habari kisiendelee na kazi, unakuwa umeathiri wengi ikiwemo wafanyakazi na hata wasomaji,’’ amesema Meena.

By Jamhuri