Na Daud Magesa,JamhuriMedia,Mwanza

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza,linawashikilia watu 21 kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili akiwemo mwenye ualbino katika wilaya za Kwimba na Sengerema.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya mauaji ya watu hao wawili kwa nyakati na matukio tofauti katika Wilaya ya Kwimba ambapo kundi la watu zaidi ya watano walimvamia na kumua Joseph Mathias ambapo wilayani Sengerema walimua mjane,Getrude Dotto.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,Kamanda wa Polisi,Wilbroad Mutafungwa amesema katika tukio la mauaji lilitokea Novemba 2,mwaka huu, majira ya usiku, ambapo watu zaidi ya watano, wanashikilia kwa tuhuma za kumuua Joseph Mathias (28).

Amesema watu hao wanadaiwa siku ya tukio walimvamia na kumshambulia marehemu Mathias (mwenye ualbino), mkazi wa Kijiji cha Ngula wilayani Kwimba,kisha kumkata kwa panga mkono wa kulia na kutokomea kusikojulikana.

Mutafungwa amesema kinara wa mauaji hayo na mmoja wa watuhumiwa hao jina linahifadhiwa,alikamatwa Novemba 6,mwaka huu, majira ya saa 6 mchana, katika Kata ya Kanyerere wilayani Misungwi,akiwa mkono wa marehemu aliokuwa ameuhifadhi kwenye begi jeusi.

“Mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na begi jeusi lililokuwa likitoa harufu ya uozo,baada ya wananchi kumtilia shaka walitoa taarifa Jeshi la Polisi ambapo alipopekuliwa alikutwa akiwa na kiungo cha binadamu (mkono) akiwa ameuhifadhi ndani ya begi,”ameeleza.

Kamanda huyo wa Polisi amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa wakati akitafuta mganga wa kumsafisha kutokana na tukio la mauaji,katika mahojiano alikiri kuhusika katika mauaji hayo na mkono huo ni wa binadamu.

Ameeleza tukio hilo la kinyama na kikatili limeacha huzuni kwa familia ambapo Polisi imejiridhisha kuwa mkono huo ni wa marehemu Mathias ambapo watapeleka sampuli kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupata uchunguzi wa kisayansi.

Kwa mujibu wa Mutafungwa jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa watano huku likiendelea kuwatafuta baadhi waliokimbia na kutahadharisha kila aliyehusika kwenye mauaji hayo hakuna atakayesalimika.

By Jamhuri