Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani
Abiri waliokuwemo katika basi la Happy Nation lililokuwa likitokea Kagera kwenda Dar es Salaam wamenusurika kifo baada ya basi hilo kupinduka upande wa kushoto eneo la Vigwaza mkoani Pwani.
Katika ajali hiyo majeruhi sita walifikishwa Hospital ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi kwa matibabu zaidi.
Akithibitisha juu ya kutokea kwa ajali hiyo wakati alipofika Hospital ya Tumbi kuwajulia hali majeruhi hao, mwenyekiti wa kamati ya usalama ya mkoa ,alhaj Abubakari Kunenge amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa 8:30 usiku Machi 2, mwaka huu.
Amesema majeruhi walikuwa idadi kubwa lakini walipata huduma kwanza katika Kituo Cha Afya Mlandizi na wengine waliruhisiwa na sita wapelekwa Hospital ya Tumbi kwa matibabu zaidi.
“Tumefika hospital ya Tumbi eneo la emergency room, tumethibitisha hospital yetu imepokea majeruhi sita hadi sasa waliotokana na ajali hiyo.
“Idadi ya majeruhi ilikuwa kubwa ambapo walikimbizwa kituo Cha Afya Cha Mlandizi na kupatiwa huduma kisha wengine waliruhisiwa kuendelea na shughuli zao nyingine ” amesema.
Kunenge ametoa rai kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kwani dereva wa basi anadaiwa kufanya uzembe kwa kutaka kulipita roli upande wa kushoto na kusababisha basi kulalia upande huo.
“Chanzo cha ajali ni baada ya dereva kutaka kulipita roli ambalo lilikuwa upande wa kushoto lakini ikashindikana na basi kupinduka upande huo.
“Tunashukuru hakuna kifo kwenye ajali hii,lakini majeruhi wapo na wengine wanaendelea kutibiwa majeraha mbalimbali na wengine wameruhusiwa kama dereva asingechukua maamuzi ya kulipita roli hilo bila kuchukua tahadhari na kufuata sheria yasingetokea haya”amefafanua Kunenge.
Naye Mganga Mfawidhi Hospital ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi, Amani Malima amesema wamepokea majeruhi sita na kuwa majeruhi hao wameumia zaidi maeneo ya mkono,mabega, mgongo lakini wanafanyiwa vipimo vya X-ray na CT-scan ili kupatiwa matibabu endapo watakuwa na madhara yatakayoonekana kitabibu.
Jeshi la Polisi mkoani Pwani limethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na, taarifa zaidi juu tukio hilo zitaendelea kutolewa.