Wizara ya Afya Zanzibar imewafutia leseni madaktari waliosababisha vifo vya mama na mtoto kutokana na uzembe walioufanya katika wodi ya wazazi Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Mei 15, mwaka huu.

Akitoa taarifa kuhusiana na hatua zilizochukuliwa dhidi ya madaktari hao kwa waandishi wa habari huko Ofisini kwake Mnazimmoja kwa niaba ya Waziri wa Afya, Naibu wa Wizara hiyo Hassan Khamis Hafidh amesema kuwa Wizara imeamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuridhika na uchunguzi uliofanywa na Baraza la Madaktari dhidi ya watendaji hao.

Aidha amefahamisha kuwa uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa madaktari hao ni wakosa kisheria akiwemo Daktari bingwa wa siku ya tukio Nihifadhi Issa Kassim ambae amefutiwa leseni kwa muda miaka miwili na hatua nyenine kufuata ikiwemo kufikishwa Mahakamani kwa kosa la jinai.

Naibu Waziri huyo amesema pia Wizara imewafutia leseni kwa muda wa mwaka mmoja na kuwafikisha Mahakamani kwa kosa la jinai Riziki Suleiman Yussuf na Salamuu Rashid Ali kwa kukiuka sheria No 17 ( 1) na sheria No 22 (1) ya sheria ya madaktari na kukiuka kiapo cha udaktari.

“Natumai sasa kwa hatua hii itakuwa ni fundisho kwa wengine kwani kuna baadhi ya watendaji wetu hawako tayari kufanya kazi wakati Serikali imapigania kutoa huduma bora kwa wananchi wake ,hivyo tutahakikisha kwa wale wote waliofanya uzembe tutawachukulia hatua kali za kisheria kwa uzembe na kusababisha vifo”,amesema Naibu Waziri.

Aidha amefahamisha kuwa kuna baadhi ya madaktari hawatekelezi majukumu yao ipaswavyo licha ya serikali kuwaongezea mishahara hivyo Wizara itawashughulikia ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zilizo bora za afya.

“Zanzibar haijawahi kumshtaki daktari kwa kufanya kosa na ndio maana makosa mengi yanafanyika kutokana na uzembe bila ya kujali uhai wa wagonjwa ,hivyo kutokana na hali hii Wizara sasa kwa makusudi imeamua kumshtaki kila atakayehusika ili kukomesha vitendo hivi.”amesema Naibu Waziri wa Afya.

Naye Mkurugenzi Kinga Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Dkt.Marijani Msafiri Marijani amewataka madaktari kubadilika na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya nane yanayodhamiria kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya Afya.

Hilo ni tukio la pili kuripotiwa katika hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja na kuchukuliwa hatua ambapo tukio la kwanza limehusisha kifo cha mtoto na Daktari aliehusika na tukio hilo alichukuliwa hatua ya kusimamishwa kazi kwa muda wa miezi sita bila ya kupatiwa mshahara wake.

By Jamhuri