Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Wakala wa Elimu Nje ya nchi Global Education Link (GEL), imeendesha zoezi la kudahili wanafunzi vyuo nje ya nchi papo hapo kwenye maonyesho ya biashara ya kimataifa yanayoendelea kwenye vuiwanja vya mwalimu Nyerere maarufu kama sabasaba.
Meneja Mkuu wa GEL, Regina Lema, amesema leo kwamba wameamua kwenda sabasaba kwaajili ya kuwadahili hapo hapo wanafunzi waliohitimu kidato cha sita wanaotaka kwenda kusoma vyuo vikuu nje ya nchi.
Alisema pia wanadahili wanafunzi waliomaliza shashahada ambao wanataka kwenda kusoma kwenye vyuo vikuu vinavyopatikana nje ya nchi.
“Kwa sasa tunadahili wanafunzi wanaotaka kwenda kuanza vyuo vikuu nje ya nchi kuanzia Septemba mwaka huu na hapa tunasajili mwanafunzi ndani ya saa 24,” amesema
“Wanaofika hapa tunawapa ushauri wa bure kuhusu taaluma wanazotaka kusomea na vyuo ambavyo vitawafaa na kozi zao na tunawaonyesha fursa zilizopo za ufadhili katika vyuo mbalimbali,” amesema
Regina aliwataka wahitimu wa kidato cha sita kuchangamkia fursa ya kwenda kwenye maonyesho ya saba saba na kutembelelea banda la Global Education Link ili kuangalia fursa mbalimbali zinazopatikana.
“Ukingia tu viwanja vya sabasaba kuna njia inakunja kushoto unaenda nayo juu tuki jirani na TRC na Chuo Kikuu Dodoma kwa hiyo hii ni fursa ya kipekee kwa wahitimu wa kidato cha sita wanaotaka kwenda nje ya nchi kwa masomo,” alisema Regina.
Kuhusu mikopo kwa wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi, Regina alisema Global Education Link wanakopesha mzazi ambaye anapaswa kurejesha ndani ya miezi nane baada ya mtoto wake kupata udahili na kwenda nje ya nchi.
Alisema mikopo hiyo haina riba kwamba mzazi anaweza kukopeshwa hadi shilingi milioni 10 na kwamba iwapo atakamilisha taratibu atapata mkopo huo ndani ya saa 24.
Regina alisema kila mwaka wanadahili zaidi ya wanafunzi 700 wanaokwenda kusoma nje ya nchi na kwamba wamekuwa wakifuatilia maendeleo yao hadi wanapohitimu.