Nape NnauyeWafuatiliaji wengi wa soka la hapa nyumbani, watakubaliana nami kuwa makocha wengi wa hapa nyumbani walioanza kufundisha soka kwenye miaka ya 1980 hadi sasa, wengi wao walipata mafunzo ya mchezo huo nje ya nchi.

Hawa ni akina Sunday Kayuni, Charles Boniface Mkwasa, Abdallah Kibadeni, Salum Madadi, Rogasian Kaijage, Juma Mwambusi, Sylvester Marsh na wengineo.

Ni katika miaka hiyo wakati nchi yetu ilipokuwa katika ubora wake katika suala zima la michezo katika ukanda huu. Hapa ndipo Watanzania walio wengi wanapomkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Ni wakati huu wa utawala wake alipoweka njia wazi kwa wanamichezo wa aina mbalimbali, kwenda kuongeza maarifa nchi za nje, hivyo wapo baadhi yao waliokwenda nchini Cuba kwa ajili ya michezo ya riadha na ngumi.

Wengine walikwenda nchini Ujerumani kupata mafunzo kwa ajili ya mchezo wa kikapu huku upande wa soka walio wengi walikwenda nchini Ujerumani na Bulgaria.

Hivi ndivyo michezo ilivyokuwa ikiendelezwa hapa nchini wakati huo wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Nyerere, na hakika matokeo yake yalionekana ndani na nje ya mipaka yetu.

Ni katika awamu hii ndipo tuliposhuhudia nchi ikitoa wachezaji mahiri katika nyanja zote za michezo hapa nchini. Kuanzia riadha tuliwaona watu kama akina Juma Ikangaa, Suleiman Nyambui, Filbert Bayi na wengine wengi.

Ukija kwenye ngumi waliowika katika mchezo huo walikuwa akina William Isangura, Titus Simba, Emmanuel Mlundwa na wengine wengi walioifanya Tanzania kuogopwa ndani na nje ya nchi.

Ni katika kipindi hiki ambapo kwa mara ya kwanza na ya mwisho timu yetu ya Taifa upande wa mpira wa miguu ilipofanikiwa kwenda kucheza mashindano ya kimataifa huko Nigeria.

Baada ya miaka mingi kupita, polepole mchezo wa soka umeanza kukosa mafanikio na hii ni matokeo ya mipango tuliyonayo ya zimamoto kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi ya juu.

Leo, pamoja na kuwa tunao makocha wengi wenye uwezo wa kufundisha soka ndani na nje ya nchi, lakini wengi wao bado wana ule utaalamu wa kizamani walioupata enzi za Mwalimu.

Mchezo wa soka ni sayansi inayobadilika kila mara. Huwezi kwenda kufundisha soka katika nchi za watu kama kwa mara ya mwisho umehudhuria kozi mwaka 1985.

Leo hii tunashuhudia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiendesha kozi fupi fupi za wiki hadi mwezi mmoja, halafu kocha huyo ndiye anayetakiwa akamwandae mchezaji wa kwenda kucheza nje ya nchi, hapa tunatarajia nini?

Sidhani kama inaingia akilini kwa kocha anayetakiwa asome kwa muda wa miezi mitatu au minne, halafu aje amwandae mchezaji kwa siku 10! Huku ni kuingiza siasa za Kitanzania ndani ya soka, mchezo unaohitaji maandalizi ya muda mrefu.

Hata hao makocha niliowataja hapo juu hakuna hata mmoja aliyepata mafunzo kwa kujilipia kwa gharama zake mweyewe, jukumu hilo lilikuwa ni la Serikali kupitia chama cha soka.

Je, kwa mipango hii ya zimamoto tunatarajia lini kuwa na makocha wanaofanya kazi nje ya mipaka yetu, au tutabaki kuwapokea akina Basena na wengine hapa nyumbani?

Kama mipango hii ya zimamoto itaendelea, hatutaweza kushindana kwenye soka na wenzetu wa ukanda huu wa Afrika, ni lazima tuwe na makocha wenye viwango bora kupata wachezaji bora watakaokuwa na uwezo wa kuvuka mipaka ya nchi yetu.

Na ikumbukwe kuwa ni sayansi ambayo kila kukicha watu wanavumbua vitu mbalimbali vinavyohitaji kocha kupata mafunzo mapya kila mara.

Ifike wakati tuwe na mipango endelevu katika soka kama kweli tunahitaji kuwa na kizazi cha soka kwa manufaa ya vijana wetu na Taifa zima kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa katika dunia ya leo soka imesaidia kuzalisha ajira kwa vijana wengi duniani na kusaidia kuinua maisha yao.

Angalia jinsi soka na michezo mingine kwa ujumla ilivyoinua maisha ya vijana wengi duniani. Watu kama Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu kwa hapa kwetu na wengine wengi, wamegeuka kuwa mabilionea kutokana na mchezo huo.

Katika dunia ambayo ajira imekuwa tatizo ni wakati mwafaka kwa Serikali kuanza kuwekeza katika soka kwa ajili ya kuzalisha ajira kwa vijana.

Ifike wakati tuache soka liwe soka kuliko kulichanganya na masuala ya siasa, ambazo nyingi ni siasa za kutafuta njia ya kujipatia fedha.

Tuachane na njia za mkato za kutaka mafanikio tusiyostahili kwa kujidanganya, tukaunda vikundi vya ushindi tukidhani kuwa tunaweza kufika tunakohitaji kwenda kwa njia ya mkato.

Sisi sote ni mashuhuda jinsi ambavyo timu yetu mara kwa mara imegeuka kuwa sawa na kichwa cha mwenda wazimu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Bara zima la Afrika kwa ujumla wake.

Ni aibu kwetu kwani katika dunia ya leo ambapo michezo imekuwa ni ajira kubwa, sisi bado tunachukulia michezo kama ni burudani tu.

Kama tunashindwa kujifunza kutoka kwa wenzetu, ni heri tukaona kwa macho baadhi ya wachezaji ambao leo wamekuwa mabilionea kupitia michezo.

Kama nilivyotangulia kueleza hapo juu, Serikali haiwezi kukwepa jukumu hili pamoja na kukabiliwa na majukumu mengine ni lazima iwekeze katika michezo.

Historia inatueleza kuwa hakuna nchi yoyote iliyopata mafanikio katika mchezo wa aina yoyote bila ya uwepo wa mikono ya Serikali ya nchi husika. Nchi kama Nigeria, Cameroon, Misri, Algeria, Senegal na nyingine nyingi zilizopiga hatua katika soka, hawakufika hapo walipo kwa bahati bali ni kwa mipango madhubuti na ya kisayansi.

Leo hii tunapozungumzia utajiri wa watu kama Samwel Eto’o, Michael Essien, Emmanuel Adebayor na wengine wengi, ni miongoni mwa watu waliohusika na mipango mizuri ndani ya nchi zao katika kuendeleza soka.

Ifike wakati Serikali yetu itambue kuwa pamoja na michezo kuwa ni burudani, lakini michezo pia ni ajira kubwa kwa vijana wengi.

Ni lazima tuanze kutumia uwezo wetu wote kuanza kuwekeza katika michezo kama tunahitaji maendeleo ya kweli, vinginevyo tusitarajie njia ya mkato kufika tunakokuhitaji.

By Jamhuri