Katika mambo ambayo yamekuwa kero kwa Watanzania kwa kipindi kirefu, ni pamoja na suala la mikataba ya siri ya uchimbaji madini, mikataba ya ufuaji umeme baina ya mashirika na Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Suala la usiri katika mikataba ya madini limewasumbua Watanzania kwa miongo miwili, tangu utawala wa awamu ya tatu. Mapema mwaka huu, Rais John Magufuli akazuia kusafirishwa kwa makontena yaliyobeba makinikia kwenda kusafishwa nje ya nchi.

Katika uchunguzi uliofanywa na Kamati Maalumu aliyoiunda Rais Magufuli, chini ya uwenyekiti wa Prof Abdulkarim Mruma, ilitoa taarifa yake na kuonesha namna nchi ilivyokuwa inaliwa na ‘mabwanyenye’. 

Hata jana tumesikia kamati nyingine iliyosheheni wanasheria  ikiwasilisha ripoti yake. Wiki iliyopita Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), imetoa tangazo la kupokea maombi ya kampuni ya kufua umeme ya IPTL kuongeza muda wa leseni kwa miezi 55, kuanzia Julai 2017 hadi Julai 2022.

Watanzania wamekuwa wanaumizwa na IPTL, kutokana na aina ya mikataba ambayo kampuni hiyo iliingia na Tanesco, tozo ya uwekezaji imekuwa kero zaidi kuliko mengine mengi. Yaani IPTL izalishe ama isizalishe umeme bado italipwa tozo ya uwekezaji kutoka Tanesco, huo ni unyonyaji usiomithilika.

Wakati IPTL inaingia mkataba huo na Tanesco, Ewura haikuwa imeundwa tayari, ila sasa inapotaka kupata leseni kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Ewura na kifungu cha 8 cha Sheria ya Umeme. Kupitia sheria hiyo, Ewura inakusanya maoni ya wadau akiwamo Tanesco, Wizara ya Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wananchi kwa ujumla.

Tunasema huu ni wakati wa Watanzania kuamua kuondokana na mikataba ya kinyonyaji, kama huo wa IPTL, ambao kwa namna moja ama nyingine ulitaka kuiyumbisha Serikali ya Awamu ya Nne. Endapo wananchi watapinga IPTL isipewe leseni na Ewura, itakuwa ni wazi kwamba tutakuwa tumeondokana na kero pamoja na kilio cha muda mrefu, huku tukishuhudia fedha za tozo ya uwekezaji zikifanya mambo mengine ya maendeleo ya nchi yetu.

Endapo taratibu za kawaida kupinga mchakato wa kuipatia leseni ya kuzalisha umeme kampuni ya kufua umeme ya IPTL, itakuwa busara mamlaka za nchi, hasa Rais Magufuli ambaye amekuwa akisimama na wanyonge, huu ni wakati wa kusimama na wanyonge.

By Jamhuri