*Asema Sh bil. 29 ni za kuibakiza madarakani

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema Sh bilioni 29 zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya Presidential Delivery Unit (Kitengo cha Kufuatilia Ufanisi wa Miradi), zitatumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha kinabaki madarakani.

Katika mahojiano maalumu na JAMHURI yaliyofanyika ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Mbowe amesema pamoja na kuiwezesha CCM kubaki madarakani, fedha hizo zitatumiwa kuhakikisha wanaondoka madarakani wakiwa “sawa sawa”.


“Ofisi ya Rais ina instrument zake zinazoongoza wizara, Ofisi ya Rais hakuna kitengo cha biashara, iweje fedha hizi zitumike kufuatilia mambo ambayo tayari yana wizara, idara na vitengo vinavyohusika?


“Huu ni mkakati wa makusudi wa kuhakikisha biashara zote kubwa zinakuwa chini ya Rais – hapa kuna gesi na miradi mingine mikubwa watakayogawana. Lakini jambo jingine ni kwamba kuundwa kwa kitengo hiki ni kukiri kwa Serikali kuwa imeshindwa, mifumo yake yote imeshindwa. Haiwezekani wizara zote zishindwe sasa Rais naye aje na kitengo.

 

“Ofisi ya Rais ni utawala, siyo biashara. Na wao siku zote wamesema Serikali haijishughulishi na biashara. Organs za Serikali zimefeli. Miradi yote ikiwa kwa rais, wizara zitafanya nini? Tatizo la nchi hii miradi inafanywa kisiasa, hakuna vipaumbele – wanaweka vipaumbele ‘viiiingi’ mwisho wa siku hakuna ufanisi. Malaysia ambako wameiga mpango huu ni tofauti na Tanzania. Viongozi wa Malaysia wana nidhamu na waliweka vipaumbele ndiyo maana wameendelea.


“Lazima uwe na vitu vinne au vitano na vifanywe ndani ya muda. Hawa (Tanzania) wana vipaumbele vitano vyenye components 24, kila mahali ahadi ya barabara – matokeo yake ujenzi wake unasuasua. Kila linalofanywa sasa na CCM hadi mwaka 2015 ni priority (kipaumbele). Wanatumia mbinu zote halali na haramu kubaki madarakani,” amesema Mbowe.


Kuna habari kwamba Sh bilioni 29 zilizoidhinishwa na Bunge, licha ya upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, zitatumika kuwalipa wataalamu watakaoletwa nchini kwa ajili ya kitengo hicho.

Hali ya mambo bungeni

Mbowe anasema hali ya vurugu iliyojitokeza bungeni kwa siku kadhaa, haiwezi kuiathiri Chadema, kwani hakuna jambo la uonevu ambalo wananchi hawajaliona.

“Wanajitahidi kulifanya Bunge liwe kama la chama kimoja. Kama hawaelewi wananchi wanasema nini, waulize kwenye vijiwe. Watu wanahoji kosa la Tundu Lissu ni nini? Kama ni la kutotii amri ya Spika ya kuketi, je, kanuni zinasemaje kuhusu adhabu? Kanuni zipo wazi kabisa, lakini kwa makusudi Kiti cha Spika kinazipindisha.


“Watu wanalalamika, wanaona tunavyoburuzwa na tunavyonyanyaswa. Hatupewi muda wa kuzungumza-kujibu hoja za uongo ambazo huibuliwa na upande wa CCM. Chunguzeni, mara zote kunapotokea vurugu bungeni chanzo huwa ni upande wa CCM.


“Shughuli bado sana hadi haki itakapotendeka bungeni…hili si Bunge la chama kimoja, wafukuzwe wote, hata abaki mmoja mapambano ya kudai haki yataendelea tu,” amesema.

By Jamhuri