*Dili ya uwekezaji yawafanya washitakiane kwa Waziri Mkuu

*Wajipanga kumkabili Kagasheki, naibu achekea kwenye shavu

Mawaziri wawili na wabunge kadhaa wameungana dhidi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kukoleza mgogoro ulioibuka Loliondo.

Mgogoro wa Loliondo unatokana na uamuzi wa Serikali, kupitia kwa Kagasheki, kumega eneo kwa ajili ya vyanzo vya maji, mapitio na mazalia ya wanyamapori. Wanaotajwa kugongana na Kagasheki kwenye sakata hili, ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Kiteto, Benedict ole Nangoro, na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye.


Wengine wanaotajwa kuwamo kwenye kundi hilo, ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, na Mbunge wa Longido, Lekule Laizer. Ingawa maeneo wanayotoka viongozi hao ni nje ya Loliondo, wote wana nasaba moja ya jamii ya wafugaji wanaoishi katika ukanda huo wa kaskazini.

Pia kuna habari kwamba Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ingawa hajiweki mbele kwenye mgogoro huo, anawasaidia naibu mawaziri hao. Kwa muda mrefu sasa, Nyalandu anatajwa kuwa hana uhusiano mzuri na Kagasheki.


Wiki iliyopita, watu waliojitambulisha kuwa ni wawakilishi wa wananchi wa Loliondo, walikwenda mjini Dodoma na kuzungumza na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.


Katika kikao chao kilichohudhuriwa na baadhi ya mawaziri na wabunge wanaotajwa kumpinga Kagasheki, yalitolewa maelezo ya sababu za wao kupinga uamuzi wa Serikali. Msimamo wao ni kwamba endapo Serikali itaendelea na msimamo wake, kutaibuka machafuko makubwa.


Hoja nyingine iliyotumiwa na watetezi hao ni kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaathiriwa kwa kukimbiwa na wanachama.


Chanzo cha habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika ofisini kwa Waziri Mkuu bungeni, kimesema Pinda hakutoa jibu la ama kutengua uamuzi wa Waziri Kagasheki, au kuendelea na msimamo huo.


Mwingine anayeshiriki kwenye sakata hilo la kupinga uamuzi wa Serikali ya CCM, ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.


Kiongozi huyo alikwishatembelea Loliondo na kutamka wazi kwamba suala hilo angelifikisha kwa Waziri Mkuu, akihofu kwamba kuendelea na msimamo uliotolewa na Serikali, licha ya kuwa ni msimamo halali kisheria, kungepunguza nguvu na umaarufu wa CCM katika eneo hilo.


Nchemba amenukuliwa akisema kwamba hata kama ni Kagasheki kujiuzulu, bora afanye hivyo. Kauli hiyo inaelekea kumfurahisha zaidi Nyalandu, ambaye walio karibu naye wanasema huenda ikamnufaisha.


Sendeka na wenzake wanaamini kuwa vijiji vya Loliondo vinastahili kuachiwa eneo lote, na Serikali isimiliki hata kilomita moja kati ya kilomita za mraba 4,000 za sasa, kwa kuwa ni Serikali hiyo hiyo iliyovipatia hati vijiji husika miaka ya nyuma na baadaye kuifuta.


Hata hivyo, inaelezwa kuwa lengo si kuwasaidia wananchi kama yalivyo maelezo yao, bali wanalenga kupata eneo hilo waanzishe mapori tengefu yanayomilikiwa na vijiji (Wildlife Management Area- WMA), kisha wawe wanapeleka wageni kufanya uwindaji wa kitalii.


Uchunguzi unaonesha kuwa hati za vijiji hivyo zilifutwa, baada ya kubainika kuwa zilitolewa kimakosa ndani ya eneo la Pori Tengefu la Loliondo, jambo ambalo ni uvunjaji wa sheria. Kwa sasa ni vijiji viwili pekee vya Ololosokwan na Ngaresero vilivyo na hati za vijiji.  Kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) ndiyo mlengwa mkuu, kwani mbali ya kunyang’anywa wastani wa kilomita za mraba 2,500, wabunge na mawaziri hawa wanapiga hesabu za mbali kuwa ikinyang’anywa na hizo kilomita za mraba 1,500 zilizosalia wanaweza kuneemeka wao.


Serikali kwa upande wake, inasema hizo kilomita za mraba 1,500 zinazosalia ni mazalia ya wanyama kama nyumbu ambao hatimaye wanasafiri na kwenda katika Mbuga ya Serengeti, hivyo kulikabidhi pori lote kwa wanakijiji na hatimaye kuanzisha hizo WMA kunaweza kuwa hatari.


Hatari inayotajwa ni kuwa vijiji vinaweza kuwinda bila mpangilio na kuharibu mazalia ya wanyama, hali inayoweza kuzifanya mbuga za Serengeti na Maasai Mara ya Kenya kupoteza umaarufu.


Eneo la Loliondo ambalo lina ukubwa wa kilomita za mraba 4,000 ni mojawapo ya mapori tengefu nchini. Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu ni kwa ajili ya matumizi ya uwindaji wa wanyamapori na shughuli nyingine za utalii.


Sehemu ya 17 ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009, inakataza shughuli za binadamu kufanyika katika maeneo hayo.


Hata hivyo, Kagasheki katika taarifa yake kwa umma, amesema; “Kwa kuwa idadi ya watu imeongezeka, mahitaji ya ardhi nayo yameongezeka katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imeona umuhimu wa kutekeleza jukumu lake la msingi kwa kutoa ardhi kwa ajili ya watu katika eneo la Loliondo.”


Kwa sababu hiyo, Serikali ilifanya uamuzi wa kuliondoa eneo la kilomita za mraba 2,500 kutoka Pori Tengefu la Loliondo na kuwapatia wananchi ili walimiliki kisheria, na kuitumia ardhi hiyo kwa shughuli za kimaendeleo.


Eneo lililobaki la kilomita za mraba 1,500 Serikali imeamua liendelee kuwa Pori Tengefu na kumilikiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009 kwa ajili ya mazalia, mapito ya wanyamapori; na vyanzo vya maji.


“Eneo hilo litaendelea kuwa chini ya Wizara, kwa kuwa linachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mfumo-ikolojia wa Serengeti. Serikali ilichukua uamuzi huo kwa kuelewa kwamba mazingira ya uhifadhi ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha mfumo-ikolojia na kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.


“Lakini baada ya uamuzi kuhusu Loliondo kutolewa, kumekuwa na maoni ya kupotosha kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), na baadhi ya wanasiasa,” amesema Kagasheki kwenye taarifa yake.


Katika kinachoonekana kama mkakati wa wabunge na mawaziri hawa, tangu Jumatatu wiki iliyopita wamekuwa wakitafutwa lakini wanagoma kuzungumza na JAMHURI, ama kwa kuomba watafutwe baadaye, au kutopokea kabisa simu zao.


Hata walipotumiwa ujumbe mfupi kwa njia ya simu kufahamishwa juu ya hali hii, inaelekea kuna makubaliano kuwa wasizungumze lolote kwani wamekaa kimya, hali inayoashiria kuwa kuna jambo linapikika.


Wakati sakata hilo likiendelea, maelfu ya ng’ombe na mifugo mingine kutoka Kenya, inaendelea kumiminika ndani ya Loliondo kwa ajili ya malisho.


Please follow and like us:
Pin Share